SUDAN

Waandamanaji nchini Sudan watishia kuuangusha Utawala wa Rais Al Bashir iwapo utashindwa kudhibiti kupanda kwa bei ya mafuta

Serikali ya Sudan inayoongozwa na Rais Omar Hassan Ahmed Al Bashir imeendelea kujikuta kwenye wakati mgumu kutokana na maandamano yanayoendelea yakiwa na shabaha ya kutaka kuangusha Serikali yake wakiituhumu imeshindwa kushughulikia matatizo yanayowakabili.

Waandamanaji nchini Sudan wakiwa katika Jiji la Khartoum na wametishia huenda wakaiangusha Serikali iwapo itakaidi kuwasikiliza
Waandamanaji nchini Sudan wakiwa katika Jiji la Khartoum na wametishia huenda wakaiangusha Serikali iwapo itakaidi kuwasikiliza
Matangazo ya kibiashara

Maelfu ya waandamanaji wameendelea kushikilia msimamo wao wa kutaka Serikali ya Rais Al Bashir iangushwe kipindi hiki ambacho maandamano yakupinga kupanda kwa ruzuku kulikochangia kuongezwa kwa bei ya mafuta na kuzua hasira kwa wananchi.

Maandamano hayo yameendelea siku nzima ya jumapili huku waandamanaji wakiwa mitaani na kupaza sauti zao kwa nguvu wakisema “Uhuru! Uhuru!” ikiwa ni shinikizo kwa Serikali ya Khartoum kuhakikisha inajibu kilio chao au inaondoka na kupisha Utawala mwingine.

Huu ni mtikisiko mwingine mkubwa unaoikumba serikali ya Sudan chini ya Rais Al Bashir ambaye alishuhudia hali kama hiyo wakati wa Machafuko yaliyoyakumba Mataifa ya Kiarabu mwaka 2011 na kusababisha tawala wa Tunisia, Misri na Libya kuangushwa.

Upinzani umekuwa mstari wa mbele kutumia maandamano haya kuhamasisha wananchi kuendelea shinikizo kwa serikali ili iweze kuleta mabadiliko ya kiutendaji na hatimaye kupunguza hali ngumu ya maisha inayowakabili wananchi wengi wa Taifa hilo.

Jeshi la Polisi kwa zaidi ya juma moja limekuwa na kibarua kigumu cha kupambana na waandamanaji waliofanya uharibifu mkubwa ikiwa ni pamoja na uchomaji wa vituo vya kuuzia mafuta na magari yaliyokuwa yameegeshwa sehemu mbalimbali.

Takwimu zimekuwa zikitofautiana juu ya watu waliopoteza maisha kwani Serikali inasema ni watu thelathini na watatu ndiyo wamepoteza maisha huku Upinzani ukisema watu wanaokadiriwa kufikia hamsini wameuawa hadi sasa.

Serikali ya Sudan imetakiwa kufanya kila linalowezekana kuhakikisha linasitisha mauaji hayo yanayoshuhudiwa kwa sasa na badala yake kusikiliza kilio cha wananchi wanaoshinikiza kupunguzwa kwa bei ya mafuta kulikokuja baada ya kuongezwa tozo ya ruzuku.