MAREKANI-ISRAELI-IRAN

Waziri Mkuu wa Israeli Netanyahu kufanya mazungumzo na Rais wa Marekani Obama juu ya mpango wa nyuklia wa Iran na amani ya Mashariki ya Kati

Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu ameelekea nchini Marekani kwa ajili ya kukutana na Rais Barack Obama katika mazungumzo ambayo yanatarajiwa kujiegemeza juu ya mpango wa nyuklia wa Iran na mazungumzo ya kusaka amani ya kudumu ya Mashariki ya Kati. Netanyahu anatarajiwa kukutana na Rais Obama kwa faragha baadaye jumatatu kabla ya jumanne kuhutubia Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa UN huku suala kubwa linalotarajiwa kuzingira mazungumzo hayo ni mpango wa Marekani kutaka kulegeza vikwazo vyake kwa Iran.

Rais wa Marekani Barack Obama akijadiliana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Rais wa Marekani Barack Obama akijadiliana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Matangazo ya kibiashara

Waziri Mkuu Netanyahu amesema atatumia nafasi yake ya mazungumzo na Rais Obama kumueleza ukweli juu ya hatua iliyopigwa na Iran katika mkakati wake wa kutengeneza bomu la nyuklia licha ya taifa hilo kuendelea kukana haijafikia hatua hiyo kwenye mpango wake wa nyuklia.

Netanyahu akiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Tel Aviv amesisitiza ukweli wake ataueleza hadi kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa UNGA ili Viongozi wa mataifa mbalimbali waweze kutambua ukweli wa kile kinachoendelea na kufanywa na Serikali ya Tehran kwa siri.

Mazungumzo kati ya Netanyahu na Rais Obama yanakuja kipindi hiki Rais wa Iran Hassan Rouhani akiwa amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Kiongozi huyo wa Serikali ya Washington na kumueleza nia yao ya kuhakikisha suluhu inafikiwa juu ya mpango wa nyuklia wa Tehran.

Netanyahu ameendelea kuonesha wasiwasi wake iwapo Iran itatekeleza kwa vitendo kauli yake ya kuwa tayari kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa juu ya mpango wake wa nyuklia huku mwenyewe akisisitiza kinachotakiwa kufanywa na Tehran ni kutangaza kusitisha mkakati wake wa kutengeneza mabomu ya nyuklia.

Waziri Mkuu Netanyahu alikosoa vikali hotuba ya Rais Rouhani aliyoitoa katika Mkutano Mkuu wa Sitini na Nane wa Umoja wa Mataifa UNGA na kusema ilijaa ubinafsi na haikuweza kueleza ni lini watasitisha mchakato wao wa kutengeza mabomu ya nyuklia ambayo ni hatari kwa usalama wa Mashariki ya Kati.

Rais Rouhani alipokelewa na maelfu ya wananchi wa Iran wakimpongeza kwa uamuzi wake aliochukua wa kukubali kushirikiana na mataifa ya magharibi juu ya mpango wake wa nyuklia wakiamini hiyo itasaidia kuondokana na vikwazo vilivyochangia kulemaza ukuaji wa uchumi wao.

Netanyahu kwa upande wake ameendelea kusisitiza kinachofanywa na Rais Rouhani hakina baraka za Kiongozi Mkuu wa Kidini Ayatollah Ali Khamenei ambaye ndiye amekuwa akisisitiza kuendelea kwa mpango wa nyuklia wa Tehran wenyewe lengo la kutengeneza silaha za maangamizi.