NIGERIA

Serikali ya Nigeria yaunda Kamati ya Kitaifa ya Majadiliano kushughulikia masuala tete ya usalama nchini humo

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan akionesha ripoti kuhusiana na utekelezaji wa demokrasia nchini mwake
Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan akionesha ripoti kuhusiana na utekelezaji wa demokrasia nchini mwake Reuters/Afolabi Sotunde

Serikali ya Nigeria imeendelea kuhaha ili kuhakikisha nchi hiyo inkuwa na utulivu na sasa imeunda Kamati ya Kitaifa ya Majadiliano ambao utasaidia kuibuka na mbinu stahiki za kuhakikisha migogoro ya kidini na mgawanyo wa utajiri wa mafuta unashughulikiwa.

Matangazo ya kibiashara

Kamati ya Kitaifa ya Majadiliano itakuwa na kazi ya kuhakikisha inaandaa mazungumzo ya kktaifa ambayo yatasaidia kukusanya maoni kutoka kwa wananchi yatakayotumika kuhakikisha masuala yenye utata yanashughulikiwa na hatimaye kuna kuwa na amani.

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ndiye ameunda Kamati hiyo akisema imekuja kwa ajili ya kuhakikisha inamaliza masuala yote yenye utata katika nchi hiyo yanayochangia uwepo wa machafuko na vifo vya raia.

Jonathan amesema Kamati hiyo imeundwa baada ya serikali kupokea mapendekezo kwa muda mrefu juu ya uwepo wa chombo kama hicho kitakachokuwa na kazi ya kuhakikisha inaitisha mazungumzo ya kitaifa mara kwa mara kujadili mambo yenye utata.

Kamati hiyo itaongozwa na Seneta wa zamani Femi Okurounmu na itakuwa na muda wa mwezi mmoja kuhakikisha imetimiza majukumu yake iliyopewa na kukusanya maoni kutoka kwa wananchi.

Kamati hiyo itazileta pamoja pande zote ambazo zinahasimiana kuanzia kwenye siasa hadi kwenye masuala ya usalama ili kuhakikisha suluhu ya matatizo yote yanafanyiwa kazi kwa wakati.

Miongoni mwa kazi nyingine ya Kamati hiyo ni kuangalia namna inayofaa katika kuhakikisha Kundi la Wanamgambo la Boko Haram linamalizwa kwani limekuwa kitisho kikubwa kwa usalama wa Taifa hilo.

Kamati hiyo pia imetakiwa kufanya kila linalowezekana ili kusaka suluhu ya tofauti ya kidini iliyojitokeza kwa wananchi wa Taifa hilo ambao wameganyika Kaskazini na Kusini kulingana na wingi wa waumini.

Eneo la Kaskazini lenye Waislam wengi limekuwa likikumbana na shinikizo kutoka kwa Boko Haram la kutaka liwe chini ya Utawala wa Sharia na hivyo kujitenga na Kusini ambako kuna waumini wengi wa Kikristo.

Serikali ya Nigeria imesema Kamati hiyo ya Kitaifa ya Majadiliano imekuja kurejesha hali ya mambo sawa kitu kitakachosaidia kukua kwa haraka kwa uchumi kunakoathirika na utengano unaoonekana.