MAREKANI

Rais Obama afuta ziara yake ya Barani Asia ili apate muda wa kushughulikia mkwamo wa bajeti ya Serikali

Rais wa Marekani Barack Obama akiendelea kutafakari njia za kushawishi bajeti mpya ya serikali kupitishwa
Rais wa Marekani Barack Obama akiendelea kutafakari njia za kushawishi bajeti mpya ya serikali kupitishwa REUTERS/Larry Downing

Rais wa Marekani Barack Obama amefuta ziara yake ya kuhudhuria mikutano miwili ya Barani Asia kipindi hiki akinyoosha kidole cha lawama kwa Wabunge wa Republican kutokana na uamuzi wao wa kukataa kupitisha bajeti mpya hatua iliyochangia kufungwa kwa shughuli za serikali za muda.

Matangazo ya kibiashara

Obama amelazimika kusitisha ziara yake kuhudhuria Mkutano wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Mataifa Asia na Pacific APEC ili aweze kupata nafasi ya kuendelea na harakati za kushawishi wabunge kupitisha bajeti mpya ya serikali ili shughuli za serikali ziweze kurejea kama awali.

Ikulu ya Marekani maarufu kama White House imesema safari zote za Rais Obama zimeahirishwa akianzia na ile ya Malaysia na ya Ufilipino kutokana na kufanya harakati za kunusuru kudorora kwa uchumi wa Taifa hilo kunakochangiwa na kusindwa kupitishwa kwa bajeti mpya ya Serikali.

Taarifa iliyotolewa na White House imethibitsha ziara zote za Rais Obama za kule Indonesia na Brunei zimefutwa mara moja na kitu pekee kinachofanyika kwa sasa ni kuhakikisha bajeti ya serikali inapitishwa na hatimaye shughuli za kawaida za taasisi hiyo kuendelea.

White House wameeleza Rais Obama amechukua uamuzi huo kutokana na kuhitaji muda zaidi wa kuendelea kushughulikia tatizo lililopo kwa sasa hivyo asingeweza kuwa nje ya Taifa hilo wakati wanapitia kipindi kigumu.

Rais Obama amesikitishwa mno na hali inayoshuhudiwa nchini mwake kwa sasa na ametoa onyo iwapo hatua hazitachukuliwa mapema basi kuna kila dalili hali ikawa mbaya zaidi katika Taifa hilo.

Obama ametaka wabunge wa Republican kutafakari kwa kina uamuzi wao wa kuendelea kushikiria msimamo mkali juu ya kupinga kupitishwa kwa bajeti mpya ya serikali kwa kisingizio cha kupingana na sheria mpya ya matibabu.

Katika hatua nyingine Shirika la Fedha Duniani IMF limeonya hatua ya Marekani kufunga shughuli zake za Serikali unaweza ukaleta madhara makubwa sana katika uchumi wa taifa hilo na dunia kwa ujuma.

Mkuu wa Shirika la IMF Christine Lagarde amesema huu ni wakati wa kunusuru hatari inayoendelea kuinyemelea nchi ya Marekani kiuchumi na hivyo lazima hatua madhubuti zichukuliwe.