MALI-UFARANSA

Uchunguzi waanza kubaini kundi lililohusika na mauaji ya wanahabari wa RFI nchini Mali

Wanahabari wa RFI waliouwawa nchini Mali
Wanahabari wa RFI waliouwawa nchini Mali RFI

Hali ya simanzi imeendelea kutanda kwenye tasnia ya habari duniani kufuatia kuuawa kikatili kwa waandishi wawili wa habari wa shirika la utangazaji la Ufaransa Radio France Internationale RFI waliouawa kwenye mji wa Kidal nchini mali wakati wakitekeleza majukumu yao. 

Matangazo ya kibiashara

Waandishi hao wa RFI Ghislaine Dupont na fundi Claude Verlon walitekwa nyara na kuuawa kwenye mji wa Kidal na kundi la wapiganaji ambao mpaka sasa hawajajipambanua.

Mkurugenzi wa Idhaa za Radio France Internationale -RFI duniani, Cecil Megie ameeleza kusikitishwa na tukio la kuuawa kwa waandishi hao na kwamba uchunguzi umeanza kubaini kundi lililohusika.

Kwa upande wake mkurugenzi wa mashirika ya utangazaji ya Ufaransa, Radio France Internationale-RFI, France 24 na kituo cha RFI kiarabu, Marie-Christine Saragosse ameeleza kuguswa na msiba huu na kwamba RFI imekuwa mfano kwenye kuripoti habari za nchini Mali na kwamba itaendelea kubaki mstari wa mbele licha ya kuwapoteza watu muhimu wakiwa mstari wa mbele.

Salamu za pole zimeendelea kutolewa na viongozi mbalimbali duniani akiwemo rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita ambaye ameahidi nchi yake kufanya uchunguzi wa kina kuwabaini wauaji hao.

Aidha serikali ya Ufaransa imesema haitaacha vita dhidi ya kutokomeza ugaidi duniani na kwamba itawalinda raia wake walioko kwenye nchi mbalimbali ambako makundi ya kigaidi yanafanya kazi zao.