UN-AU-ICC-KENYA

Hatma ya kesi za Kenya kwenye mahakama ya ICC kujulikana hii leo baada ya kura ya Baraza la Usalama

Mwendesha mashtaka wa mahakama ya ICC Fatou Bensouda
Mwendesha mashtaka wa mahakama ya ICC Fatou Bensouda Reuters

Mataifa ya Afrika hii leo yanaingia katika mtihani mkubwa wa kujaribu kuwashawishi wajumbe wa nchi wanachama wa baraza la usalama kwenye Umoja wa Mataifa kuwalazimisha wapige kura kushinikiza mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC kuahirisha kesi za viongozi wa Kenya kwa mwaka mmoja zaidi. 

Matangazo ya kibiashara

Mataifa ya Afrika yamewasilisha ombi maalumu kwenye baraza la usalama la umoja huo kutaka wajumbe wake wapige kura kuishinikiza mahakama ya ICC kuahirisha kesi za uhalifu dhidi ya binadamu zinazomkabili rais wa Kenya, uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto.

Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa licha ya kuwasilishwa kwa azimio hilo la nchi za Afrika kwenye baraza la usalama, bado kuna nafasi ndogo ya nchi hiyo kuungwa mkono pendekezo lao kwakuwa halikuungwa mkono pia na nchi nyingi duniani.

Tayari kesi dhidi ya naibu wa rais William Ruto imeshaanza kwenye mahakama ya ICC huku ile ya rais Kenyatta ikitarajiwa kung'oa nanga mwezi February mwakani huku tayari nchi hiyo ikiwa ya kwanza kuwasilisha ombi la kutaka kesi zao ziahirishwe.

Kwa mujibu wa sheria inayotambua mkataba wa Roma ulioanzisha mahakama ya ICC, nchi wanachama zinaweza kutumia kifungu namba 16 cha mkataba huo kuiagiza mahakama hiyo kuahirisha kesi hizo kwa mwaka mmoja zaidi.

Hili ni jaribio la kwanza kubwa zaidi kuwahi kufanywa na nchi za Afrika kwenye Umoja wa Mataifa kutaka kuahirishwa kwa kesi zinazoendelea kwenye mahakama ya ICC jambo ambalo ni wazi wachambuzi wa mambo wanaona kuwa litaleta hali ya sintofahamu ndani ya nchi wanachama kuhusu kesi hizo.

Haya yanajiri wakati utafiti uliofanywa na kampuni ya utafiti ya Synovet nchini Kenya, ukionesha kuwa wananchi wengi wanaunga mkono rais Kenyatta kuhudhuria kesi yake pamoja na nchi hiyo kutojitoa kwenye mkataba wa Roma unaotambua mahakama hiyo.