LEBANONI-IRANI

Shambulizi kubwa latekelezwa nje ya ubalozi wa Iran nchini Lebanoni

REUTERS

Milipuko mikubwa miwili imetokea leo jumanne nje ya ubalozi wa Iran mjini Beirut nchini Lebanoni na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 20 na kujeruhi wengine zaidi ya 140, polisi na vyombo vya usalama wamethibitisha. Vyombo vya habari nchini humo vinasema mlipuko huo umetokea karibu na ngome ya wanamgambo wa kundi la Hezbollah, eneo ambalo tayari limekumbwa na milipuko mara mbili kwa mwaka huu wa 2013.

Matangazo ya kibiashara

Wanausalama wanasema milipuko hiyo imesababishwa na roketi mbili zilizorushwa katika eneo hilo, wakati chanzo kingine cha usalama kimesema milipuko hiyo imetokana na bomu la kutegwa kwenye gari.

Kundi la Jihad la Abdullah Azzam Brigades lenye uhusiano na mtandao wa kigaidi duniani wa al-Qaeda limekiri kuhusika na shambulizi hilo. Magaidi hao kupitia mtandao wa twitter wamesema tukio hilo ni ujumbe wanaotaka ufikie Iran na kundi la Hezbollah.

Magari, miti na majengo katika eneo hilo yameharibika vibaya, na juhudi za uokoaji zinaendelea ili kuwasaidia manusura na pia kutafuta miili ya watu wengine waliopoteza maisha.

Hospitali ya jirani ya Zahraa imesema tayari imepokea maiti kadhaa na majeruhi wanaoendelea kupatiwa matibabu mpaka hivi sasa.

Mshauri wa utamaduni katika ubalozi wa Iran nchini humo Sheikh Ibrahim Ansari ni miongoni mwa watu waliopoteza maisha katika shambulizo hilo, amefariki baada ya kufikishwa hospitali kutokana na majeraha aliyopata wakati shambulizi hilo lilipotekelezwa muda aliokuwa anaingia ubalozini.

Hali ya usalama nchini Lebanoni bado tete kutokana na mzozo wa nchi jirani ya Syria, na kundi la Hezbollah limekuwa likikosoa waumini wa Kisunni wa Lebanoni wanaounga mkono mharakati za kumuondoa madarakani Rais wa Syria Bashar al-Assad.