Uganda-Afrika ya Kati

Wanajeshi wa Uganda wawatia mbaroni waasi 19 wa kundi la Lords Resistance Army

Waasi wa kundi la Lords Resistance Army LRA
Waasi wa kundi la Lords Resistance Army LRA www.naharnet.com

Wanajeshi wa Uganda wamewatia mbaroni waasi 19 wa kundi la uasi la Lords Resistance Army nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR)Umoja wa Afrika umebainisha tukio ambalo ni la ushindi wakati huu waasi hao wakisakwa kila kona. 

Matangazo ya kibiashara

Jeshi la Uganda linaongoza jeshi la Umoja wa Afrika linaloungwa mkono na Marekani , katika jukumu la kuwakamata viongozi wa kundi la LRA, wengi wao wakitakiwa na mahakama ya kimataifa ya ICC huko Hague Uholanzi kwa makosa ya uhalifu wa kivita.

Wafuasi hao 19 wa kundi la LRA waliochini ya kundi linaloongozwa na Luteni Kanali Obur Nyeko alia Okuti, waliasi na kujisalimisha kwenye kundi la Uganda mnamo Disemba 6 , Umoja wa Afrika umeeleza kwenye taarifa yake iliyotolewa jana Jumanne.

Mwezi uliopita Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilielezea wasiwasi wake kuhusu ghasia nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati huenda zikavuruga kutafutwa kwa kiongozi wa waasi wa kundi la LRA Joseph Kony ambaye anatuhumiwa kwa vifo vya watu laki moja kwenye ukanda huo.

Kony ambaye alianzisha uasi nchini Uganda miongo miwili iliyopita, anatafutwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC sambamba na makamanda wake wa juu kwa makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu yakiwemo mauaji , utumwa wa ngono na kutumia watoto wadogo kwenye jeshi lake.