SOMALIA

Abdiwel Sheikh Mohamed ateuliwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa Somalia

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mahmud amemteua mtaalamu wa uchumi Abdiweli Sheikh Mohamed kuwa Waziri wake mkuu mpya ili kukomesha hali ya kuzorota kisiasa wakati huu nchi hiyo ikikabiliana na changamoto za usalama unaotetereshwa na kundi la kigaidi la alshabab.

Matangazo ya kibiashara

Uteuzi huo unalenga kuziba nafasi iliyokuwa ya Abdi Farah Shirdon ambaye alivuliwa madaraka hayo na bunge baada ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Mogadishu, Rais Mahmud amesema Sheikh Mohamed anakidhi vigezo vya kushika wadhifa huo na anaamini bunge litamuidhinisha bila vikwazo.

Endapo bunge litaridhia uteuzi wa Mohamed, atakuwa na muda wa siku 30 kuteua baraza lake la Mawaziri ambalo nalo itabidi liidhinishwe na bunge.

Awali Sheikh Mohamed amewahi kufanya kazi na taasisi mbalimbali za kimataifa ikiwemo benki ya maendeleo ya kiislamu nchini Saudi Arabia.

Mohamed mwenye umri wa miaka 54 anakabiliwa na kibarua cha kupambana na rushwa, vita dhidi ya Al-Shabaab na kulijenga upya taifa hilo la pembe ya Afrika.