Syria-Kemikali

Ban Ki-moon: Waliohusika na matumizi ya silaha za kemikali huko Syria wawajibishwe

REUTERS/Kacper Pempel

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN ban Ki-moon ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwawajibisha waliohusika na mashambulizi ya silaha za kemikali nchini Syria. Katibu Mkuu Ban ameliambia Baraza la Usalama la umoja huo UNSC kuwa ni lazima hatua zichukuliwe kwa waliohusika kwani vitendo hivyo ni kinyume na haki za binadamu.

Matangazo ya kibiashara

Ripoti ya UN ya alhamisi juma hili ilibainisha kuwa silaha hizo zilitumika takribani mara tano toka serikali ya Damascus kuridhia uamuzi wa kuteketezwa kwa maghala yake ya silaha.

Hata hivyo ripoti ya wataalamu wa kemikali wa UN haikuweka bayana upande upi ulitumia silaha hizo.

Kiongozi wa Jopo la wataalamu waliofanya kazi hiyo Ake Sellstrom alisema hana mamlaka ya kumnyooshea kidole mtu yoyote na kwamba vigezo hivyo vinaweza kutumiwa na watu wenye mamlaka hayo.

Kwa mujibu wa makubali yaliyopo hivi sasa inabidi uteketezaji wa silaha za Syria ukamilike katikati ya mwaka ujao wa 2014.

Mataifa ya Magharibi, serikali za Kiarabu, Makundi ya kutetea haki za binadamu na waasi wa Syria wamekuwa wakiishutumu serikali ya Rais Bashar al-Assad kuhusika na matumizi ya silaha hizo. Lakini Rais Assad na washirika wake iwemo Iran nao wamekuwa wakiwatupia mpira waasi.