MAREKANI-Mashariki ya kati

Marekani iko mbioni kuhakikisha Israel na Palestina zinafikia mkataba wa amani

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry anafanya ziara ya kikazi katika ukanda wa mashariki ya kati, ziara yenye kuwa na matumaini ya kuwashawishi viongozi wa Israeli na Palestina kufikia mkataba wa amani.Hii itakuwa ni ziara ya kumi ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani nchini Israeli na eneo la Scijordania yenye lengo la kutafuta amani baina ya Israeli na Palestina kupitia njia ya mazungumzo.

Matangazo ya kibiashara

Baada ya pande hizo mbili kuonyesha nia ya kurejea kwenye meza ya mazungumzo katika mwaka uliopita wa 2013, kisha kusitishwa kwa majadilinao kwa kipindi cha miaka mitatu, John Kerry anapania kuanza mwaka huu wa 2014 na hari isiokuwa ya kawaida ili kuhakikisha ndugu mahasimu wanapatana.

Kwa kipindi kirefu kiongozi wa mamlaka ya wa Palestina pamoja na waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu wamekuwa wakifanya mazungumzo ya chini kwa chini, lakini sasa wakati umewadia wa kuweka bayana mazungumzo hayo,  ili pande zote mbili zielewe nini kinachoendelea kabla ya kupatikana kwa mkataba wa amani.

Pande hizo mbili zimekutana zaidi ya mara ishirini katika mazungumzo ya moja kwa moja tangu Julay mwaka 2013, na zipo tayari kuendelea kujadiliana hadi mwezi April.

Wakati muda wa kufikia mwisho wa mazungumzo hayo ukikaribia na hakuna hatuwa kubwa ambayo imekwisha pigwa, licha ya Israeli kuwaachia huru hapo jana wafungwa raia wa Palestina, na hii ndio imekuwa sababu ya waziri wa mambo ya nje kufanya ziara katika eneo hilo ili kuendelea kuwashawishi viongozi wa pande hizo mbili.

Ziara hii ya John Kerry mashariki ya kati, inakuja siku moja baada ya rais wa Mamlaka ya wa Plaestina Mahmoud Abbas, kutishia kuchukuwa hatuwa za kisheria na kidiplomasia ili kuhakikisha Israeli inasitisha ujenzi katika maeneo ya walowezi wa kiyahudi.