UFARANSA

Padri Georges Vandenbeusch apongeza juhudi zilizopelekea anatoka mikononi mwa waliyomteka

Padiri Georges Vandenbeusch, Amewasili nchini Ufaransa mapema leo asubuhi, baada ya kutekwa mateka kwa kipindi cha mwezi moja na nusu nchini Cameroon. Vandenbeusch, amewashukuru wale wote waliyokua wakiendesha ibada mbalimbali ili aweze kutoka mikononi mwa watekaji nyara, huku akiwapa moyo wale ambao bado wamo mikononi mwa watu hao.

Matangazo ya kibiashara

“Siku hii, imekua kama ndoto kwangu, lakini ikilinganishwa na mateka waliyobali kipindi kirefu mikononi mwa watekaji nyara, inanionyesha ni jinsi gani mateka hao wako katika matatizo magumu”, amesema Padri Vandenbeusch.

Kumesalia kwa sasa raia sita wa Ufaransa, ambao wanashikiliwa mateka duniani: wawili katika jangwa la Sahel na wanne nchini Syria.

Padri Vandenbeusch, alitekwa nyara kaskazini mashariki mwa Cameroon na kundi la waislamu wenye itikadi kali la Boko Haram, katikati mwa mwezi wa novemba, na baadae kuziwiliwa nchini Nigeria.

Padri Georges Vandenbeusch, amepongeza taasisi mbalimbali za taifa la Ufaransa, ambazo kila upande ulijitahidi vya kutosha ili aweze kutoka mikononi mwa watekaji nyara.

Baada ya mkutano na waandishi wa habari, akiwa pamoja na rais wa Ufaransa François Hollande, ambae alikuja kumlaki, padri Georges Vandenbeusch atapelekwa kwenye hospitali ya kijeshi ya Val-de-Grâce mjini Paris kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya.

Padri Georges Vandenbeusch mwenye umri wa miaka 42 , alitekwa nyara na wanamgambo waliojihami kwa silaha nzito mnamo Novemba 13, baada ya kumvamia parokiani kwake majira ya usiku.

Kundi la wanamgambo wa kiislam wenye msimamo mkali Boko Haram , ambalo limeua maelfu ya watu katika mashambulizi dhidi ya wakristo na serikali Kaskazini mwa Nigeria, lilikiri kumshikilia mateka padri huyo mara tu baada ya kutekwa kwake.