LEBANON

Makao makuu ya Kundi la Hezbollah nchini Lebanon yakabiliwa na shambulizi ya hapa na pale

Takriban watu watano wamepoteza maisha nchini Lebanoni katika shambulio lililotokea jana alhamisi kusini mwa jiji la Beyrouth, ikiwa ni shambulio la nne kutokea katika kipindi cha miezi sita makao makuu ya kundi la Hezbollah yakilengwa. Tangu kundi la Hezbollah lilipojiunga na majeshi ya serikali ya rais Bashar Al assad nchini Syria kupambana na waasi wanaoipinga serikali, kundi hilo limekuwa likilengwa katika mashambulizi mbalimbali ya kujitowa muhanga.

Matangazo ya kibiashara

Taifa la Lebanoni halina serikali tangu kipindi cha miezi nane kufuatia mgawanyiko wa wanasiasa nchini humo kuhusu mzozo wa Syria, ambapo kundi la Hezbollah lenye wafuasi wa madhehebu ya washia na upande mwingine wa Saad Hariri wa madhehebu ya wa Sunni.

Baada ya kutokea kwa shambulio hilo kundi la Hezbollah limewatolea wito wananchi wa taifa hilo kuwaunga mkono, ili kuepusha mgawanyiko wa nchi, wito ambao umetupiliwa mbali na muungano wa Saad Hariri unaolituhumu kundi hilo kuhusika katika mauaji ya Mohamed Chatah, mmoja kati ya viongozi wa muungano siku ya ijumaa iliopita. Tuhuma ambazo Hezbollah imekanusha.

Kwa mujibu wa waziri wa mambo ya ndani Marwan Charbel, uchunguzi unaonyesha kwamba ni shambulio la Kigaidi kufuatia kukutwa kwa vipande vya mwili wa binadamu katika gari lililotumiwa katika mlipuko huo.

Jeshi la Lebanoni, limethibitisha kwamba gari hilo aina ya Jeep Cherokee lilikuwa limebeba kilogram ishirini ya vilipuzi.