SUDANI KUSINI-Ethiopia-Mazungumzo

Mazungumzo ya kusaka amani Sudan Kusini yanatazamiwa kuanza rasmi baada ya kusuasua kwa siku mbili zilizopita

Serikali ya Ethiopia imesema kua mazungumzo ya kusaka amani katika taifa changa la Sudan Kusini, ambalo linakabiliwa na mapigano kwa zaidi ya majuma mawili sasa kati ya jeshi linalomuunga mkono rais wa nchi hio, Salva Kiir, na aliekua makamo wake, Riek Machar. Wajumbe kutoka pande zote mbili, inaarifiwa kua, wamewasili mjini Addis Ababa, nchini Ethiopia.

Matangazo ya kibiashara

Hata hivo, jeshi la Sudani Kusini limesema kwamba linaelekea kuukomboa mji muhimu wa Bor ulioangukia mikononi mwa waasi wanaomuunga mkono aliyekuwa makamo wa rais wa taifa hilo Riek Mashar, wakati mazungumzo baina ya serikali ya Juba na waasi ambayo yalitarajiwa kuanza  yakiendelea kusuasua.

Msemaji wa jeshi la Sudani Philip Aguer amesema awali waliondoka katika mji huo, kwa sababu za kujipanga, na sasa wapo tayari kuurejesha kwenye himaya ya serikali.

Vikosi vya waasi wanaomtii, Riek Masha, jumanne ya juma hili viliuteka mji wa Bor ulipo kwenye umbali wa kilometa mia mbili pekee na mji mkuu wa Juba.

Tangu kuanza kwa mapigano majuma mawili yaliyopita, mji huo wa bor umetekwa na waasi mara tatu.

Pande zote mbili husika na mzozo huo zipo jijini Addis Abeba nchini Ethiopia kwa ajili ya mazungumzo, lakini hapo jana, wameshindwa kuanzisha mazungumzo na kupanga agenda ya mazungumzo hayo.

Yohanis Musa Pouk mjumbe wa waasi katika mazungumzo hayo alisema kwamba wamekuja kuzungumza lakini hawajawa tayari kukutana na upande wa serikali.

Mzozo huo wa nchini Sudani Kusini umekuwa ukionyesha sura ya mzozo wa kikabila, lakini wachambuzi wa siasa wanaona kuwa sio wa kikabila bali ni wa kisiasa.

Mashirika ya misaada ya kibinadamu yametahadharisha juu ya kuendelea kushuhudiwa kwa hali mbaya kwa raia wasiokuwa na hatia na kuomba pande zote mbili zinazo gomba, kusitisha mapigano na kuanzisha mazungumzo mara moja.