IRAQ

Majeshi ya Iraq yapoteza udhibiti wa mji wa Fallujah baada ya kuzidiwa nguvu na wanamgambo

Majeshi ya serikali ya Iraq yamepoteza udhibiti wa mji muhimu wa Fallujah ambao umeangukia mikononi mwa wapiganaji wenye uhusiano na mtandao wa kigaidi duniani wa Al Qaeda. Maeneo ya Ramadi na Fallujah, magharibi mwa mji mkuu wa nchi hiyo Baghdad, yamedhibitiwa na wanamgambo kwa siku kadhaa kama ilivyotokea mwaka 2003 baada ya Majeshi ya marekani kuvamia maeneo hayo wakati yalipokuwa ngome kuu za wanamgambo hao.

REUTERS/Stringer
Matangazo ya kibiashara

Waziri Mkuu wa nchi hiyo Nouri Al Maliki amesema majeshi yake yanaendelea kupambana na wanamgambo hao ili kuwaondoa kabisa katika jimbo la Anbar.

Zaidi ya watu mia moja wameuawa katika makabiliano makali kati ya polisi wa Iraq na kundi la wanamgambo ambalo wamechukua udhibiti wa jimbo la Anbar na kutangaza kuwa taifa la kiislamu.

Mapigano yalianzia huko ramadi baada ya majeshi ya usalama kuziondoa kambi za waandamanaji zilizofunguliwa baada ya kuanza kwa maandamano dhidi ya kile ambacho wasuni wanadai kuwa ni kulengwa kwa jamii yao.

Hasira dhidi ya serikali inayoongozwa na Washia miongoni mwa Wasuni ilionekana kuwa kichocheo cha vurugu zilizoikabili Iraq kwa takribani miaka 5.