SUDANI KUSINI-Mazungumzo

Mazungumzo ya kusaka amani Sudan Kusini kuanza jumapili hii Addis Ababa nchini Ethiopia

REUTERS/James Akena

Mazungumzo ya ana kwa ana baina ya pande zinazohasimiana nchini Sudani Kusini yanatarajiwa kuanza leo jumapili jijini Addis Ababa nchini Ethiopia. Wajumbe wa Rais Salva Kiir na wale wa aliyekuwa makamu wake Riek Machar waliwasili Addis Abab takribani siku tatu zilizopita lakini hawakuweza kuanza mazungumzo hayo wakisubiri ajenda ya majadiliano ambayo walitaka kwanza ikubaliwe na pande zote.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mazungumzo hayo, Waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia Tedros Adhanam amesema Sudani Kusini inahitaji amani na maendeleo na sio vita kama inavyoshuhudiwa hivi sasa, na amewataka wajumbe wa pande zote kuhakikisha wanatumia nafasi ya mazungumzo kwa umakini ili kuhakikisha suluhu inapatikana.

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton amepongeza hatua ya pande zote kukubali kwenda katika meza ya majadiliano na ameziomba pande zote kujiepusha na kauli za kichochezi ambazo huenda zikavuruga mchakato huo.

Wakati huo huo Nchini Sudani Kusini mapigano yameendelea kushuhudiwa, Msemaji wa Jeshi la serikali Phillip Aguer amesema vikosi vyao vinazidi kusonga mbele kuelekea mji wa Bor ambao umekuwa ukidhibitiwa na waasi kwa mara ya tatu.

Machafuko hayo yamesababisha watu zaidi ya laki mbili kuyakimbia makazi yao na watu zaidi ya elfu moja wamepoteza toka mapigano hayo yalipoanza katikati ya mwezi Desemba mwaka jana.