JAMUHURI YA KIDEMOKRASIA YA CONGO-MAZISHI

Wananchi wa Kaskazini mwa DRCongo waendesha ibada sanjari na wale wa Kinshasa katika mazishi ya Kanali Mamadou N'Dala Moustafa wakati wanajeshi kadhaa wakitiwa nguvuni

Mazishi ya Kanali Mamadou N'Dala Mustapha aliyeuawa Alhamisi juma lililopita mjini Beni Jimboni Kivu Kaskazini baada ya kushambuliwa na waasi wa Uganda ADF NALU, yatafanyika leo Jumatatu mjini Kinsasha. Kanali huyo ambaye alipendwa sana na waakazi wa Jimbo la Kivu Kaskazini kutokana na ukakamavu wake na kuongoza jeshi la serikali kuwashinda waasi wa M23 mwaka uliopita amezikwa pamoja na askari wengine tisa wakiwemo walinzi wake wawili na wengine waliouawa jijini Kinshasa mwishoni mwa mwaka uliopita.

Mazishi ya kanali Mamadou Ndala Mustapha
Mazishi ya kanali Mamadou Ndala Mustapha
Matangazo ya kibiashara

Kanali Mamadou Ndala aliuawa kwa kupigwa roketi ndani ya gari alililkuwemo na kundi la watu ambao serikali inasema ni waasi wa kundi la Uganda la ADF-NALU wakati ambapo tayari wanajeshi kadhaa wa jeshi la FARDC wametiwa nguvuni kwa kushukiwa kuhusika na mauaji hayo.

Kamanda wa jeshii katika mji wa Beni Luteni Kanali Tito Bizuru alikamatwa akijaribu kutoroka wakati huu uchunguzi ukiendelea kuhusu mauji ya Ndala.

Siku ya Jumamosi wananchi wa maeneo ya mkoa wa kivu ka kaskazini waliandamana kudai kiongozi huyo wa operesheni za kijeshi mashariki mwa DRCongo azikwe katika eneo hilo, jambo ambalo serikali ilitupilia mbali na kuamuwa kumfayia mazishi yake huko Kinshasa.

Mashirika ya kiraia mashariki mwa DRCongo yamewatolea wito wananchi wa maeneo hayo kutoelekea katika shughuli zao wa kila siku ili kumuenzi shujaa huyo ambaye walimchukulia kama mkombozi dhidi ya waasi wa M23.

Mamadou Ndala, alikuwa kwenye mstari wa mbele katika mapambano makali na vikosi vya FARDC vilivyosaidiwa na majeshi ya Umoja wa Mataifa yaliyowango’a waasi wa M23, aliuawa pamoja na walinzi wake wawili.

Awali msemaji wa serikali ya Congo, Lambert Mende, alilituhumu kundi la waasi wa ADF kuhusika na kifo cha afisa huyo wa jeshi la Congo kanali Mamadou Ndala

Wanaharakati wa haki za binadamu mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wameomba uchunguzi uanzishwe haraka iwezekanavyo ili waliyohusika na kifo cha Mamadou Ndala Moustafa wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.

Serikali ya DRC, pamoja Na askari 21,000 wakulinda amani kutoka Umoja wa Mataifa, wanaendelea kujaribu kuyaangamiza makundi ya waasi mashariki mwa nchi hiyo.

Kanali Ndala alijulikana sana katika eneo hilo baada ya kikosi alichokiongoza kupata ushindi mara kadhaa dhidi ya waasi wa kundi la M23 ambalo Rwanda na Uganda zinatuhumiwa kuunga mkono kundi hilo lililotanga Novemba 5 mwaka jana kuachana na uasi baada ya kukabiliwa vikali na mashambulizi ya vikosi vya FARDC.