JAMUHURI YA AFRIKA YA KATI

Mkutano wa kutafakari hali ya usalama nchini Jamuhuri ya Afrika ya Kati unapangwa kufanyika hivi karibuni

Mwezi mmoja baada ya kuanza kwa operesheni Sangaris ya jeshi la Ufaransa, serikali ya Chad imethibitisha kuandaa mkutano maalum wa nchi za Jumuiya ya kiuchumi Afrika ya Kati utakaofanyika Ijumaa, tarehe 9 Januari mjini N'djamena kuhusu usalama nchini Jamuhuri ya Afrika ya Kati. Mkutano huo utalenga kujadili maendeleo katika mipango ya usalama tangu operesheni ya kulinda amani nchini jamhuri ya Afrika ya Kati ianzishwe. 

Matangazo ya kibiashara

Mbali na mkutano huo, kutakuwa pia na mkutano mwingine wa Kimataifa mwezi ujao, kuhusu namna ya kuijenga upya nchi hiyo utakaofanyika jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Umoja wa Mataifa unaonya kuwa mzozo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati unakaribia kuwa janga.

Umesema nusu ya idadi ya watu wameachwa bila makaazi katika mzozo wa kikabila, ambao ulizuka tena mwezi uliopita.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa karibu watu milioni mbili laki mbili wanahitaji msaada wa dharura wa kiutu, na kwamba nusu ya wakaazi wa mji mkuu Bangui, wameachwa bila makaazi.

Watu zaidi ya laki moja wanasemekana kuishi katika kambi ya muda karibu na uwanja wa ndege mjini humo.

Taifa hilo lilitumbukia katika mgogoro mwezi machi mwaka jana, wakati mapigano yalipozuka baina ya makundi ya wapiganaji wa Kikiristo na Kiislamu.

Waasi wa Kiislamu walitwaa madaraka kupitia mapinduzi, ambayo kiongozi wa sasa Michael Djotodia alichukua nafasi ya Rais Francois Bozize.

Tayari mataifa mbalimbali yameanza kuhamisa raia wao.

Mali na Senegal zimewahamisha mamia ya raia wao wanaotoroka mapigano ya kimadhehebu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Zaidi ya watu 200 wamesafirishwa hadi mji mkuu wa Mali, Bamako, huku ndege ya pili ikitarajiwa kuisafirisha idadi sawa na hiyo kurejea Mali hii leo.

Senegal imesema imewahamisha raia wake karibu 600 katika kipindi cha juma moja. Senegal pia iliwahamisha raia wa Guinea na Gambia.

Mwishoni mwa wiki, Nigeria ilisema inawaondoa nchini humo zaidi ya raia alfu moja mia sita waliokimbilia kwenye ubalozi wake katika mji mkuu Bangui.

Wakati huohuo, Jenerali Mohamed Moussa Dhaffane ambaye ni kiongozi wa zamani wa kundi la waasi wa seleka ameachiwa huru baada ya kifungo cha miezi sita chini humo.