MAREKANI-SYRIA

Marekani kuwashiwishi waasi wa Syria kushiriki mazungumzo ya pili ya Geneva

REUTERS/Brendan Smialowski

Marekani imejipanga kuendelea kushinikiza wapinzani nchini Syria kushiriki mazungumzo ya pili ya Ganeva yanayotarajiwa kuanza tarehe 22 mwezi huu. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry anajiandaa kuelekea jijini Paris Ufaransa ambapo kesho jumapili atakutana na Mawaziri toka nchi zinazowaunga mkono waasi wa Syria, wanaojiita marafiki wa Syria katika jitihada za kuhitimisha maswala muhimu kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo.

Matangazo ya kibiashara

Mkutano huo utawakutanisha Mawaziri toka nchi za Uingereza, Misri, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Jordan, Uturuki, Saudi Arabia, Jumuiya ya Falme za Kiarabu na Marekani.

Mkuu wa Baraza la upinzani la Syria Ahmad Jarba ni miongoni mwa wajumbe watakaohudhuria mkutano huo.

Waasi wa Syria walitoa msimamo wa kutoshiriki mazungumzo ya amani mpaka pale Rais Bashar al Assad atakapoachia madaraka, lakini serikali ya Damascus inasisitiza kuwa suala la Assad kuondoka madarakani halitawezekana.

Maelfu ya watu wameuawa toka machafuko hayo yalipozuka mwezi machi mwaka 2011 wakati waasi walipoanzisha harakati za kumng'oa madarakani Rais Assad.