JAMUHURI YA AFRIKA YA KATI

Milio ya risasi yatikisa mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati baada ya serikali ya mpito kujiuzulu

REUTERS/Herve Serefio

Milio ya risasi imesikika katika mitaa mbalimbali ya mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Bangui saa chache baada ya kutangazwa kwa habari za kujizulu kwa Rais wa mpito wa Taifa hilo Michel Djotodia, aliyekabiliwa na shinikizo la kimataifa kuachia ngazi baada ya kushindwa kudhibiti machafuko ya kidini yaliyosababisha umwagikaji mkubwa wa damu.

Matangazo ya kibiashara

Baada ya kutangazwa kwa habari hizo, maelfu ya wananchi waliingia mitaani kusherekea uamuzi huo, lakini saa chache baadae ilisika milio ya risasi hewani ingawa haijafamika ni kundi gani lililofanya kitendo hicho.

Kujiuzulu kwa Djotodia na Waziri wake Mkuu Nicolas Tiangaye kulitangazwa jana ijumaa katika mkutano wa siku mbili wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika ya Kati nchini Chad.

Baraza la kitaifa nchini Jamhuri ya Afrika ya kati ambalo ndilo bunge la mpito nchini humo, linakutana mjini N'djamena kabla ya kuendelea na kikao jijini Bangui kujadili juu ya kuwateuwa viuongozi wapya wa taifa hilo.

Wajumbe wa Baraza hilo la kitaifa nchini Jamhuri ya Afrika ya kati ambao walialikwa kwenye mkutano huo wataidhinisha hatua ya kujiuzulu kwa rais Djotodia na baadae kuwatafuta viongozi wengine.

Rais Djotodia alichukua madaraka mwezi Machi mwaka jana wakati aliposaidiwa na wapiganaji wa Seleka waliofanikisha kumuondoa madarakani aliyekuwa Rais wakati huo Francois Bozize.