UMOJA WA MATAIFA-SUDANI KUSINI

Rais wa Sudani Kusini ahimizwa kuwaachia wafungwa wa kisiasa ili kufanikisha mazungumzo ya amani

Reuters/Stringer

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki-moon, na Baraza la usalama la umoja huo UNSC wamemuomba Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir kuwaachia wafungwa wa kisiasa ili kusaidia jitihada za upatikanaji wa amani kupitia mazungumzo ya Addis Ababa nchini Ethiopia.

Matangazo ya kibiashara

Ban Ki-moon amesema juma hili amezungumza na Rais Salva kiir kumhimiza awaachie wafungwa hao ili kurejesha matumaini ya kusitishwa kwa mapigano yaliyosababisha kuuawa kwa maelfu ya watu toka vita ilipoanza katikati ya mwezi desemba mwaka jana.

Baraza la usalama la UN pia limemuhimiza Rais Salva Kiir kuwaachia waasi wanaoongozwa na makamu wake wa zamani Riek Machar ili kurahisisha mazungumzo ya kusaka amani huko jijini Addis Ababa.

Riek Machar ameendelea kusisitiza kwa serikali ya Juba kuwaacha huru wafungwa 11 wanaotuhumiwa na serikali ya Sudani Kusini kufanya jaribio la mapinduzi ili kuendelea na mazungumzo, jambo ambalo Serikali ya Rais Kiir imeshindwa kutekeleza.

Hayo yanajiri wakati majeshi ya Serikali na yale ya waasi wakiendelea kupambana huko Sudani Kusini, huku shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi duniani UNHCR likisema kwamba linatarajia kuwapokea wakimbizi laki nne kutoka Sudani Kusini badala ya laki mbili na elfu thelathini.

Siku ya ijumaa wanajeshi wa taifa hilo walisema wamechukua udhibiti wa mji wa Bentiu ambao ulikuwa ukidhibitiwa na waasi watiifu kwa aliyekuwa makamu wa Rais wa nchi hiyo Riek Machar.