JAMUHURI YA AFRIKA YA KATI-Wito

Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati awataka raia walio ukimbizini kurudi makwao

RFI

Rais wa Mpito wa Jamhuri ya Afrika ya kati Alexandre Ferdinand Nguendet amewataka wakimbizi wa ndani walioko maeneo ya Uwanja wa ndege mjini Bangui na wapatao elfu mia moja kurudi nyumbani, akiwahakikishia usalama wao wakati ambapo askari wa Ufaransa na vikosi vya Afrika wakiendelea na jukumu lao la kuwapokonya silaha makundi ya wapiganaji na kulinda amani.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mara ya kwanza baada ya wiki kadhaa za makabiliano, wapiganaji wa pande zote mbili mjini Bangui wameamua jana kusitisha uhasama hali ambayo inaweza kuvunjika wakati wowote.

Wakati huo huo, Bunge la mpito nchini humo litakuwa na kibarua kigumu kuanzia kesho kumteuwa rais mpya wa mpito baada ya kujiuzulu kwa Mitchel Djotodia wiki iliyopita.

Hayo yakijiri, vurugu kubwa pamoja na taarifa za ulaji wa nyama za watu na uporaji mkubwa zimeripotiwa kuzuka mjini Bangui mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati baada ya kujiuzulu kwa rais wa taifa hilo na kiongozi wa zamani wa waasi Michel Jotodia ambaye ameelekea Benin jana Jumamosi.

Michel Djotodia aliwasili katika mji mkuu wa Benin ambako kunatajwa huenda akakaa uhamishoni baada ya kujiuzulu wadhifa wake chini ya shinikizo la kidiplomasia siku ya Ijumaa,kufuatia kukithiri kwa vurugu mjini Bangui ambapo kujiuzulu kwake kulitoa matumaini ya kutuliza mvutano uliopo.

Saa kadhaa baada ya kujiuzulu kwake takribani watu watano waliuawa katika usiku uliotawaliwa na milio ya risasi kulingana na takwimu mpya zilizotolewa na shirika la Msalaba Mwekundu nchini humo.