Umoja wa Mataifa nchini DRCongo wasema Kundi la waasi la M23 limeanzisha mchakato wa kusajili wapiganaji wapya nchini Rwanda na Uganda

RFI

Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Monusco umesema hautokubali kuanzishwa kwa operesheni za kijeshi za kundi la waasi wa M23 na wataendelea kuwapiga vita pamoja na makundi mengine. Kiongozi wa Majeshi ya Umoja wa Mataifa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Munusco, Martin Kobler amesema kuwa waasi wa kundi la M23 wanaweka mikakati ya kurejea tena Mashariki mwa nchi hio.

Matangazo ya kibiashara

Kobler ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jijini New York kuwa kwa sasa waasi hao wanapewa mafunzo na nchi za Rwanda na Uganda walikokimbilia.

“Baada ya kulitokomeza kijeshi kunda la M23, sasa ni muda wa kutekeleza azimio la Nairobi kwa vile vyanzo vinavyoaminika, vinabaini kuwa kundi hilo linaendelea kusajili waasi wengine baada ya azimio hilo, pia vyanzo vingine vimebaini harakati za M23 kwenye maeneo ya Ituri kaskazini-mashariki mwa DRC.

Natoa wito kwa serikali ya Rwanda na Uganda kuzuwia M23 waliokimbila huko kuendelea na mafunzo ya kijeshi katika nchi hizo kwa sababu hatutovumilia waasi wa M23 waanze upya harakati zao”, amesema Kobler.

Wakati huohuo hali ya usalama imekua ikidorora katika baadhi ya maeneo ya mashariki mwa jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mashirika ya kiraia Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yanasema idaidi ya viongozi wa serikali za mitaa wanaouliwa mashariki mwa nchi hiyo hasa mjini Beni yanaendelea kushuhudiwa .

Wilayani Watalinga viongozi watano wameuwawa katika kipindi cha miezi sita iliyopita.