JAMUHURI YA AFRIKA YA KATI-Bunge

Rais mpya wa mpito wa Jamhuri ya Afrika kati anatazamiwa kuteuliwa na Bunge la mpito

RFI

Bunge la mpito la Jamhuri ya Afrika ya Kati litakutana hii leo katika zoezi maalum la kuweka ratiba ya uteuzi wa Rais mpya wa mpito. Hata hivyo, chama cha rais wa zamani Francois Bozizé tayari kimelituhumu Bunge kutokuwa na uwakilishi wa nchi nzima kwa vile linajumuisha wabunge waliochaguliwa na aliyekuwa rais, Michel Djotodia na waziri wake mkuu , Nicolas Tiangaye, tuhuma ambazo bunge linakanusha.

Matangazo ya kibiashara

Leah Koyassoum kaimu spika wa bunge la Jamhuri ya Afrika ya kati, amesema Francois Bozizé, asitaki kupotosha raia na Jumiya ya Kimataifa.

“Watu wanao haki ya kuzungumza lakini sisi tunaendelea na kazi, wasitake kutupotezea muda.

Wawakilishi wa Francois Bozize wako ndani ya Bunge na naweza hata kutaja majina yao, wapo hapa. Kwa hiyo ikiwa wana jambo la kuzungumzia walizungumzie kwa njia ya wawakilishi wao. Hatuwezi kupoteza muda kwa kusikiliza malalamiko ya kila mmoja wao”, amesema Koyassoum .

Wakati huohuo, Mamia ya askari waliotoroka jeshi miezi ya hivi karibuni wameanza kurejea kambini kwa kuitikia wito wa rais wa muda Alexandre-Ferdinand Nguende.

Jenerali Ferdinand Bombayake ni Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Afrika ya Kati, ameomba Jumuiya ya Kimataifa kuwasaidia kuunda jeshi litakalo jumuisha koo zote.

“Hamna budi Jumuiya ya Kimataifa kutusaidia kujenga jeshi kwa kujumuisha wote kwa vigezo vya uuwiano wa kikabila, majimbo, umri, elimu na uzalendo ili kujenga jeshi ambalo litakuwa kwa ajili ya maslahi ya kitaifa na sio ya mtu binafsi”, amesema jenerali Bombayake.

Rais Nguendet anatazamiwa kuongoza leo jumaini kikao maalumu cha Baraza la Kitaifa la Mpito, ambacho kinao muda wa siku 15 ya kumteuwa rais mpya wa mpito, ambae atakua mgombea kwenye uchaguzi wa urais baada ya kipindi cha miezi sita katika mwaka 2015.

Duru kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati, zinafahamisha kwamba ,kunahitajika wagombea zaidi ya kumi, na bwana Nguendet atakua miongoni.

Nguendet anapewa kipao mbele kuchukua wadhifa huo, kulingana na idadi kubwa ya wabunge (135) wanaomuunga mkono.