LEBANON-Sheria

Kesi ya mauaji ya waziri mkuu wa zamani nchini Lebanon yaanza kusikilizwa

RFI

Kesi dhidi ya wanachama wanne wa kundi la Hezbollah wanaotuhumiwa kutekeleza mauji ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Lebanon Rafik Hariri mwaka 2005 imeanza katika Mahakama Maalumu ya Umoja wa Mataifa mjini Hague nchini Uholanzi. Ni miaka tisa tangu kuuawa kwa Waziri Mkuu Hariri mjini Beirut yeye pamoja na watu wengine 22 baada ya kushambuliwa na washukiwa hao ambao hawako Mahakamani.

Matangazo ya kibiashara

Mwanaye Rafik Hariri Saad Hariri ambae pia aliwahi kuwa waziri mkuu naye pia alikuwa mjini Hague wakati kesi hio ilipofunguliwa jana na kusema kuwa ana imani haki itatendeka ili waliomuua babake wachukuliwe hatua.

Mahakama inayisikiliza kesi hiyo, ambayo ni ya kipekee kwa sababu inaweza kuendelea licha ya kutokuwepo kwa washukiwa hao wanaoshakiwa kuhusika na makosa tisa likiwemo lile la ugaidi na uuaji.

Mahakama maalumu iliyoundwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2007 (STL) kushughulikia kesi ya mauaji ya waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Rafiq Hariri ilitoa mwaka 2011 ripoti iliyoonesha kuhusika kwa viongozi wanne wa Hezbollah na mauaji ya kiongozi huyo.

Katika ripoti hiyo ambayo pia ilichapishwa kwenye tovuti ya mahakama ya umoja wa mataifa inayoshughulikia kesi hiyo iliweka wazi makosa matano ambayo yanawakabili watuhumiwa wanne wa chama kinachotawala hivi sasa nchini humo Cha hezbollah kwa kuhusika kwao katika mpango wa mauaji ya waziri mkuu rafiq Hariri.

Viongozi waliotajwa kwenye ripoti hiyo ni pamoja na Mustafa Amine Badreddine, Salim Jamil Ayyash, Hussein Hassan Oneissi na Assad Hassan Sabra ambao kwenye ripoti hiyo wameelezewa jinsi walivyoshiriki katika kuandaa mpango wa kutekeleza shambulio la kumuua kiongozi huyo.

Miongoni mwa makosa ambayo wanashtakiwa nayo viongozi hao ni pamoja na kushiriki vitendo vya kigaidi na kuandaa njama za kutaka kuipindua serikali iliyokuwa ikiongozwa na waziri mkuu Rafiq Hariri.

Mwezi wa sita mwaka 2011 mahakama hiyo ilitoa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa viongozi hao na kufikishwa mbele ya majaji kujibu tuhuma za mauaji zinazowakabili.

Kundi la Hezbollah kupitia kwa msemaji wake lilikataa kushirikiana na mahakama hiyo.

Hata hivyo wachambuzi wa masuala ya sheria za kimataifa waliwahi kukosoa ripoti hiyo wakidai kuwa ina mapungufu kwa kuwa ilishindwa kuwahusisha maafisa wa usalama wa nchi ya Israel ambao wanatajwa pia kuhusika katika kusuka mpango wa mauaji ya Rafiq Hariri.

Waziri mkuu wa Rafiq Hariri aliuawa mwezi wa pili mwaka 2005 ambapo baada ya kifo chake mtoto wake Saad Hariri alichukua madaraka kabla ya kushuhudia pia hata yeye mwenyewe akilazimika kuondoka madarakani kwa shinikizo la chama cha Hezbollah.