SYRIA-Mazungumzo

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani autaka upinzani kushiriki mazungumzo kati yake na serikali

RFI

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry ameuomba muungano wa upinzani nchini Syria kuhudhuria mazungumzo ya amani yatakayofanyika mwezi ujao mjini Gevena nchini Uswisi. Wito huu unakuja wakati huu muungano huo wa upinzani ukikutana mjini Istanbul leo Ijumaa kupiga kura kuamua ikiwa utahudhuria mazungumzo hayo kati yao na serikali ya rais Bashar Al Assad.

Matangazo ya kibiashara

Kerry amesema mazungumzo hayo ya Geneva ni muhimu sana, kwani yataweka mipango ya kuunda serikali ya mpito ili kumaliza machafuko yanayoendelea nchini Syria.

“ Ni muhimu kila upande uje kwenye meza ya mazungumzo ili suluhu lipatikane”, amesema Kerry.

Muungano wa upinzani umekuwa ukisema hauwezi kuketi katika meza moja na rais Assad na unamtaka ajiuzulu ili washiriki katika mazungumzo hayo.

Hayo yanajiri wakati wafadhili na marafafiki wa Syria walikutana nchini Kuwait na kuahidi kutoa ahadi ya dola bilioni 2 nukta 4 kusaidia hali ya Kibinadamu nchini humo kutokana na machafuko yanayoendelea.

Wajumbe kutoka Mataifa Sabini duniani na Mashirika 24 ya Kimataufa walikutana jumatano chini ya uongozi wa katibu mkuu Ban Ki Moon ambaye alisema ahadi iliyotolewa haikufikia nusu ya fedha zinazohitajika ambazo ni zaidi ya dola Bilioni 6 kuwasaidia raia wa syria wanaoishi katika mazingira magumu.

Takriban nchi 24 zilikutana pamoja na masharika ya kimataifa chini ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon. Umoja wa Mataifa umesema, unahitaji dola za marekani bilionni 2.3 ili kuwasaidia watu milioni 9.3 raia wa Syria na dola za Marekani bilioni 4.2 kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi ambao wanakadiriwa kufikia milioni 4.1 katika mwaka huu wa 2014.

Awali, kamishana wa Umoja wa Ulaya anaye husika na misaada ya kibinadamu Kristalina Georgieva alisema Umoja wa Ulaya utaongeza idadi yake ya msaada wa euro milioni 165 kwa waathirika wa machafuko, huku akitolea wito Jumuiya ya Kimataifa kufuata mfano wa Umoja wa Ulaya, ambayo yao pekee imeitolea msaada nchi ya syria wa euro bilioni 2 tangu mwanzoni mwa machafuko.

Machafuko ya Syria yameingia katika mwaka wa tatu, na yamesababisha zaidi ya watu laki moja kupoteza maisha na mamilioni kuyahama makaazi yao.