THAILAND-Maandamano

Maandamano makubwa zaidi dhidi ya serikali ya Thailand kufanyika hii leo

Reuters

Waandamanaji wanaoipinga serikali ya Thailand wamepanga kufanya maandamano makubwa zaidi hii leo katika mji mkuu wa nchi hiyo Bangkok, siku moja tu baada ya shambulizi la bomu kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa waandamanaji Suthep Thausguban anatarajiwa kuongoza harakati hizo, huku wapinzani wakisema wataandaa timu ya ulinzi ili kujilinda baada ya kiongozi wao kunusurika katika mlipuko wa jana.

Utawala nchini Thailand pamoja na upinzani wote wanatupiana lawama kuhusiana na tukio hilo ambalo inadaiwa kitu cha mlipuko kilirushwa kutoka kwenye eneo moja jirani na eneo ambalo waandamanaji wa upinzani walikuwa wamekusanyika.

Nchi ya Thailand imejikuta kwenye hali mbaya kisiasa toka kupinduliwa kwa waziri mkuu wa zamani Thaksin Shinawatra miaka 7 iliyopita na sasa mdogo wake, Yingluck Shinawatra anakabiliwa na shinikizo la kujiuzulu akituhumiwa kuongoza nchi kwa kuzingatia matakwa ya ukoo wake.

Hofu imezidi kutanda nchini humo kufuatia shambulizi la hivi karibuni ambalo ni miongoni mwa matukio mabaya kushuhudiwa tangu kuanza kwa harakati za kuipinga serikali ya Yingluck.

Yingluck ameitisha uchaguzi mkuu mwezi ujao wa Februari, lakini wapinzani wanapinga upigaji kura wakihofia ushidni kushikiliwa tena na familia ya Shinawatra.