SUDANI KUSINI-UN

Umoja wa Mataifa UN walaani utumikishwaji wa watoto kwenye makundi yanayopigana nchini Sudani Kusini

Umoja wa Mataifa UN umesema una ushahidi kuwa watoto wamekuwa wakitumikishwa kama wanajeshi katika mapigano yanayoendelea nchini Sudani Kusini. Naibu Katibu Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa Ivan Simonovic amesema idadi kubwa ya watoto wamesajiliwa katika kundi la wapiganaji wanaojiita Jeshi Jeupe kutoka kabila la Nuer linalopigana kwenye jimbo le Jonglei.

REUTERS/James Akena
Matangazo ya kibiashara

UN imesema utaendeleza uchunguzi ili kubaini maswala hayo sambamba na mauaji ya kiholela, utekaji nyara, unyanyasaji wa kijinsia na ukiukwaji mwingine wa haki za binadamau unaotokana na vita hivyo.

Mapigano nchini humo yalizuka toka katikati ya mwezi Desemba mwaka jana baada ya serikali ya Rais Salva Kiir kumshutumu makamu wake wa zamani Riek Machar kutaka kufanya jaribio la mapinduzi dhidi ya serikali yake.

Pande mbili zinazokinza zipo katika mazungumzo ya kutafuta suluhu jijini Addis Ababa Ethiopia, lakini mazungumzo hayo yamekuwa yakiendelea kwa mwendo wa kinyonga.

Miongoni mwa madai ya waasi yanayokwamisha mazungumzo hayo ni kutaka wafungwa wa kisiasa wanaoshikiliwa na serikali waachiwe huru, lakini serikali ya Juba imekuwa ikikataa kutekeleza matakwa hayo.