JAMHURI YA AFRIKA YA KATI-Usalama

Kikosi cha wanajeshi wa Umoja wa Afrika kiko tayari kuhakikisha usalama umerejea nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati

Baadhi ya wanajeshi wa kikosi cha wanajeshi kutoka mataifa ya Afrika Misca, mjini Bangui
Baadhi ya wanajeshi wa kikosi cha wanajeshi kutoka mataifa ya Afrika Misca, mjini Bangui RFI

Licha ya kuanza kurejea kwa hali ya utulivu kwenye baadhi ya maeneo nchini Jamhuri ya Afrika ya kat,i bado kumeripotiwa vurugu na mauaji ya wenyewe kwa wenyewe kwenye miji mingi ambayo inakaliwa na wakristo. Vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika MISCA vimekuwa na kazi ya ziada kuyadhibiti baadhi ya makundi ya vijana wa Kikristo kaskazini mwa nchi hiyo kwenye mji wa Boali ambao wamekuwa wakitekeleza mauji dhidi ya waumini wa dini ya kiislamu kwa madai ya ulipizaji kisasi dhidi ya ndugu zao waliouawa.

Matangazo ya kibiashara

Mkuu wa operesheni za kijeshi za majeshi ya MISCA nchini humo, Jenerali, Jean Marie Michel Mukoko anasema kuwa kwa sasa wanalenga kuhakikisha usalama mjini Bangui kabla ya kuelekeza nguvu zaidi kwenye maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo ambako kuna mapigano yanaripotiwa.

Katika hatua nyingine bunge la mpito nchini humo leo hii linatarajiwa kupigia kura majina 8 yaliyowasilishwa bungeni na hatimaye kupata jina moja la kiongozi ambaye atakuwa rais wa mpito.

Hata hivyo bado kunashuhudiwa mgawanyiko mkubwa ndani ya kundi la waasi wa Seleka waliohusika kufanya mapinduzi nchini humo.

Umoja wa mataifa umeonya kuhusu kuendelea kushuhudiwa kwa mauji ya ulipizaji kisasi nchini humo dhidi ya waumini wa dini ya kiislamu.