MISRI-Kura ya maoni

Umoja wa Ulaya wapongeza zoezi la kura ya maoni kuhusu katiba mpya nchini Misri

Raia wanounga mkono utawala, mjini Cairo wakionyesha furaha yao
Raia wanounga mkono utawala, mjini Cairo wakionyesha furaha yao RFI

Umoja wa Ulaya EU umedokeza kuridhishwa na namna zoezi la kura ya maoni kuhusu katiba mpya nchini Misri lilivyoendeshwa na kuongeza kuwa hizi ni hatua za awali kuelekea demokrasia ya kweli nchini humo. Mkuu wa Sera za mambo ya nje wa Umoja huo, Catherine Ashton amesema kuwa wameridhishwa na jinsi kura hiyo ilivyofanyika na kutoa wito kwa upinzani nchini humo kuheshimu maamuzi ya wananchi.

Matangazo ya kibiashara

Lakini wakati Umoja wa Ulaya ukipongeza kura hiyo, upinzani nchini Misri ambao ulisusia kushiriki kwenye kupiga kura kupitisha rasimu ya katiba, wameendelea kusisitiza kuwa kura hiyo ilikuwa ni yawazee na sio vijana wambao kwa sehemu kubwa walishiriki kuuangusha utawala wa Hosni Mubarak miaka mitatu iliyopita.

Wakati huohuo Marekani imeitaka hivi karibuni nchi ya Misri kusimamia kwa makini utekelezaji wa katiba mpya iliyoungwa mkono na asilimia 98.1 ya wananchi waliopiga kura.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema mataifa mbalimbali yanataka kuona Misri inatumia katiba yao kujiimarisha kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa maslahi ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Serikali ya mpito imepongeza wananchi waliounga mkono katiba mpya ikisema maamuzi hayo yanaashiria kuunga mkono hatua ya jeshi kumpindua rais Mohamed Morsi.

Mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Sisi, jenerali ambaye aliongoza mapinduzi ya Morsi, alikuwa akifuatilia matokeo ili kupata ishara ya kuunga mkono uwezekano wa jitihada za urais.

Katiba hiyo mpya inachukua nafasi ya katiba iliyopitishwa mwezi Disemba mwaka 2012 chini ya rais Morsi, ambapo ilipata theluthi mbili ya kura zote huku asilimia 33 ya raia wakijitokeza kupiga kura.