SYRIA-Mazungumzo

Upinzani nchini Syria watichia kutoshiriki mazungumzo ya kusaka amani

Mkuu wa muungano wa upinzani nchini Syria, Ahmed Moaz al-Khatib
Mkuu wa muungano wa upinzani nchini Syria, Ahmed Moaz al-Khatib RFI

Muungano wa upinzani nchini Syria umesema huenda usirishiriki mazungumzo ya Geneva namba mbili iwapo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa UN, Ban ki Moon hatobatilisha uamuzi wake wa kuialika nchi ya Iran kwenye mazungumzo hayo. Kauli ya Muungano wa upinzani nchini Syria inakuja ikiwa zimepita saa chache toka katibu mkuu wa Umoja wa mataifa, Ban Ki Moon atangaze kutumia mamlaka yake kama msuluhishi mkuu wa mgogoro huo kuialika nchi ya Iran.

Matangazo ya kibiashara

Katibu mkuu Ban amesema kuwa nchi ya Iran inamchango mkubwa kwenye kumaliza machafuko ya nchini Syria na kwamba waziri wake wa mambo ya kigeni wa Iran, Mohammad Javad Zarif ameahidi kutoa mchango chanya kwenye mazungumzo hayo.

katibu mkuu Ban mbali na kuialika nchi ya Iran, pia ametoa mwaliko kwa ujumbe wa kanisa katoliki toka Vatican pamoja na taasisi nyingine za kidini kushiriki kwenye mazungumzo ya tarehe 22 mwezi huu.

Awali viongozi wa Mataifa ya Magharibi walipongeza hatua ya wapinzani nchini Syria kukubali kushiriki mazungumzo ya amani ya kimataifa yanayolenga kutafuta suluhu ya machafuko yaliyodumu kwa miezi thelathini na nne.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry alipongeza uamuzi huo na kusema ni mwanzo wa njia ngumu ya kutafuta suluhu.

Uingereza, Ufaransa na Ujerumani nao walipongeza hatua hiyo iliyofikiwa baada ya majuma kadhaa ya hofu na vitisho vya kususia mazungumzo hayo kutoka kwa wapinzani.

Mazungumzo ya pili ya Geneva yamepangwa kuanza nchini Uswisi jumatano tarehe 22 ya mwezi huu, lakini wapinzani wanasema lengo lao kuu ni kumwondoa madarakani rais Bashar Al Assad.

Upande wa Rais Assad umekubali kushiriki mazungumzo hayo lakini umesema kamwe kiongozi wao hatoachia madaraka mpaka pale wananchi wake watakapofikia maamuzi hayo.