MISRI-Maandamano

Maandamano ya kumuunga mkono Abdel fattah el-Sisi kugombea kiti cha urais yafanyika Misri

Abdel Fattah Al-Sisi, waziri wa ulinzi wa Misri akiwa pia mkuu wa majeshi
Abdel Fattah Al-Sisi, waziri wa ulinzi wa Misri akiwa pia mkuu wa majeshi RFI

Maelfu ya wananchi wa Misri wanaomuunga mkono kiongozi wa kijeshi nchini humo, wameandamana hapo jana kumshinikiza kiongozi wao kuwania kiti cha urais kwenye uchaguzi mkuu ujao. Abdel fattah el-Sisi, mkuu wa majeshi na waziri wa ulinzi aliyeshiriki kumpindua rais Mohamed Morsi amekuwa gumzo miongoni mwa wananchi wa taifa hilo ambao wanaunga mkono uamuzi wake wa kumpindua rais Morsi ambapo kwenye maandamano ya hapo jana wameendelea kusisitiza kiongozi huyo kugombea urais.

Matangazo ya kibiashara

Maandamano hayo yaliyoongozwa na aliyekuwa waziri wa ulinzi, Ahmed gamal Eddin, amewaambia waandamanaji kuwa kwa taifa hilo kuendelea kidemokrasia ni lazima jenerali el-Sisi awanie kiti cha Urais na si vinginevyo.

Kupitishwa kwa katiba mpya ya nchi hiyo kwenye kura ya maoni iliyopigwa juma moja lililopita, ni wazi sasa kunampa nafasi jenerali el-Sisi kuwa na uwezo wa kuwania nafasi ya urais kwa mujibu wa katiba hii, jambo ambalo wachambuzi wa mambo wanaona kuwa kiongozi huyo atawania urais.

Katika hatua nyingine, mfadhili mkubwa wa rais wa mpito nchini Misri, Mustaf Hegazy amewaambia waandishi wa habari wa vituo vya kimataifa mjini Cairo, kuwa taifa hilo kamwe haiwezi kurejea kwenye utawala wa kizamani ambao ulikuwa umekithiri kwa rushwa na utawala wa kimabavu.