UKRAINE-Maandamano

Rais wa Ukraine aapa kutong'atuka madarakani

Maandamano zaidi yameendelea kushuhudiwa nchini Ukraine, wakati huu nchi ya Urusi ikionya kuwa huenda machafuko hayo yakaifanya serikali kushindwa kuwa na udhibiti.Maelfu ya waandamanaji wa upinzani wameendelea kukaidi tangazo la serikali kuwataka kuondoka kwenye viunga vya mji mkuu Kiev na badala yake waandamanaji hao wanakabiliana na polisi.

REUTERS/Valeriy Bilokryl
Matangazo ya kibiashara

Mamia ya watu wameripotiwa kujeruhiwa na wengine kukamatwa na vyombo vya usalama, hali inayomfanya mkuu wa tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Matiafa, Navi Pillay kupitia msemaji wake kuitaka nchi ya Ukraine kuheshimu haki za binadamu.

Rais wa Ukraine, Viktor Yanukovich ameendelea kusisitiza kwamba hang'atuka madarakani na badala yake anashinikiza upinzani kuachana na maandamano na kurejea kwenye meza ya mazungumzo.

Waziri wa Mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov aliwashtumu jana baadhi ya wanasiasa barani Ulaya kuchochea machafuko nchini Ukraine.

Lavrov alisema ikiwa uchochezi huo utaendelea hali itaendelea kuwa mbaya nchini humo kutokana na machafuko yanayoendelea kwa sasa.

Hapo juzi polisi wa kutuliza ghasia mjini Kiev waliendelea kukabiliana na maelfu ya waandamanaji wa upinzani wanaoshinikiza kujiuzulu kwa rais Yanukovich.

Waandamanaji nchini humo wamekasirishwa na hatu ya rais Viktor Yanukoych kwa kutoingia katika Mkataba wa kibiashara na Umoja wa Ulaya.

Rais Yanukovich ameahidi kuzungumza na upinzani na waandamanaji hao ili kufikia muafaka.

Rais wa Ukraine, Viktor Yanukovich amewaonya waandamanaji mjini Kiev na kuwataka kuondoka kwenye maeneo wanayoyakalia wakati huu maelfu ya polisi wakipelekwa kudhibiti hali ya usalama.

 

Mwanzoni mwa mwezi desemba, mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi wanachama wa NATO walikashifu utumizi wa nguvu kupita kiasi unaotumiwa na maafisa wa usalama kupambana na waandamanaji wanaotaka kujiuzulu kwa serikali.

Mawaziri hao waliitaka serikali ya Ukraine kusikiliza sauti ya wananchi wake na kuacha kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji hao.