SYRIA-Mazungumzo

Mazungumzo ya kusaka amani nchini Syria yaanza nchini Uswisi

wajumbe katika kikao
wajumbe katika kikao

Ujumbe wa viongozi wa muungano wa Upinzani wa Syria na ule wa Serikali ya rais Bashar al-Asad ukiongozwa na waziri wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo tayari wamewasili mjini Geneva kwa mazungumzo ya amani. Punde mara baada ya kuwasili, upinzani umekuwa na mazungumzo ya faragha na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ambapo wameendelea kusisitiza kuondoka madarakani kwa rais Asad kupisha mchakato wa kupatikana kwa amani nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Kwa upande wake waziri Muallem amesema suala la rais Asad kuondoka madarakani ni jambo ambalo haliwezekani na upinzani usitarajie kuona kiongozi huyo akitekeleza jambo hilo.

Katika hatua nyingine, katibu mkuu wa Umoja wa mataifa UN Ban Ki Moon akifungua mkutano wa kimataifa kuhusu kuoinga matumizi ya silaha za kemikali, ameitaka dunia kupinga kwa nguvu zote matumizi ya silaha hizo akitolea mfano kile kilichotokea nchini Syria.

Hayo yakijiri, mawakili wa kimataifa wametaka kushtakiwa kwa rais wa Syria Bashar al-asad pamoja na maofisa wengine kwenye Serikali yake, kufuatia ripoti iliyotolewa juma hili ikionesha picha za kutisha ya namna ambavyo vyombo vya usalama nchini humo vinavyohusika na ukiukaji wa haki za binadamu.

Kwenye ripoti ya uchunguzi iliyofadhiliwa na Serikali ya Qatar, imeorodesha makosa yaliyotekelezwa na maofisa wa Serikali ya Syria ambao wamehusika na kuwatesa maelfu ya wafungwa.

Ripoti hiyo inaeleza kwa kina namna ambavyo utesaji huo ulivyofanyika na namna rais Asad anavyohusika na kutoa maelekozo kwa maofisa wake kutekeleza vitendo hivyo.

Katika hatua nyingine kumeripotiwa mapigano kwenye maeneo mbalimbali ya nchi wakati huu ambapo hii leo mazungumzo ya ana kwa ana kati ya viongozi wa Syria na wale wa waasi wanakutana kwa mazungumzo mjini Geneva.