Syria - Mapigano

Mapigano yajitokeza nchini Syria wakati mazungumzo ya amani yakiendelea

wajumbe katika mazungumzo ya Syria
wajumbe katika mazungumzo ya Syria REUTERS/Jamal Saidi

Mapigano makali yameripotiwa nchini Syria kwenye mji wa Allepo na miji iliyoko mpakani mwa nchi hiyo na Uturuki saa chache baada ya kufunguli wa rasmi kwa mazungumzo ya amani ya mjini Geneva. Kwa mara ya kwanza viongozi wa utawala wa rais Assad ulikutana ana kwa ana na upinzani nchini Syria kwenye mkutano ambao pande hizo mbili zimeendelea kushutumia kwa kushiriki vitendo vya mauji dhidi ya raia wasio na hatia.

Matangazo ya kibiashara

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanaona kuwa mapigano yanayoripotiwa hivi sasa nchini Syria yanatia dosari mazungumzo yanayofanyika mjini Geneva.

Serikali ya Marekani kupitia waziri wake wa mashauri ya kigeni, John Kerry, imeendelea kusisitiza kuwa itawaongezea nguvu wapiganaji wa upinzani nchini Syria katika harakati zao za kuhakikisha rais Assad anaondoka madarakani.

Hapo jana wakati wa ufunguzi wa mkutano huo nchi ya Urusi imeonya kuhusu nchi zinazoendelea kutoa silaha kwa makundi yanayopigana nchini Syria, huku ikieleza kusikitishwa na hatua ya nchi ya Iran kutoshirikishwa kwenye mazungumzo hayo.

Mataifa makubwa duniani yamewatolea wito waasi wa Syria na serikali kutumia fursa hadimu na ya kihistoria ya mazungumzo ya awamu ya pili ya mjini Geneva kukomesha machafuko ya zaidi ya miaka mitatu sasa.

Hata hivyo viongozi hao wametofautiana kuhusu undwaji wa serikali ya mpito ambapo Marekani inasema rais Assad hawezi kupewa mamlaka ya kuwaongoza wananchi ambao amekuwa akiwateketeza kwa kuwashambulia kwa mabomu, jambo ambalo Urusi imeupilia mbali.