SUDANI KUSINI-Mazungumzo

Wajumbe wa Sudani Kusini wanaelekea kusaini makubaliano ya kusitisha vita katika mazungmzo ya jijini Addis Ababa

RFI

Wajumbe wa serikali ya Sudani Kusini na wale wa waasi katika mazungumzo ya amani na kusitisha mapigano yanayolikumba taifa changa la Sudan Kusini tangu Desemba 15 mwaka 2013, wanaelekea kusaini hii leo makubaliano ya usitishwaji mapigano mjini Addis-Ababa, baada ya kuvutana kwa muda wa siku kadhaa.

Matangazo ya kibiashara

Wajumbe wa serikali ya Sudan Kusini na wale wanaomtii aliekuwa makamu wa rais, Riek Machar, wamekuwa wakizungumza kwa shida tangu mwanzoni mwa mwezi wa jJanuari katika mji mkuu wa Ethiopia, chini ya uongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Afrika ya Mashariki (Igad), ambayo inaundwa na mataifa saba

Jumuiya hiyo imetoa tangazo, ambamo imebaini kwamba kutakuepo na sherehe za kutia saini kwenye mkataba baadaye leo jioni.

Wawakilishi wa pande mbili watasaini nyaraka mbili, ambapo moja ni ya usitishwaji mapigano kati ya jeshi la Sudan Kusini linalomtii rais Salva Kiir na waasi wanaomuunga mkono Riek Machar, na nyingine ya kuachiwa huru wanasiasa 11 washirika wa karibu wa Riek Machar, ambao wanaziwiliwa jela tangu mapigano yalipozuka kati ya jeshi mjini Juba desemba 15.

Rais Salva Kiir anamtuhumu makamu wake kwamba alijaribu kuipindua serikali yake bila mafanikio.

Kwa upande wake, Riek Machar anatupilia mbali tuhuma hizo, akibaini kwamba hizo ni mbino za Salva Kiir za kutaka kuwamalizia maisha wapinzani wake, ambao wote ni kutoka kundi la zamani la waasi wa kusini waliyoendesha vita dhidi ya Khartom tangu mwaka 1983-2005, ambavyo vilipelekea taifa hilo kupata uhuru wake.

Mapigano yaliyoenea nchi nzima yamesababisha maelfu ya raia kupoteza maisha na mamilioni kuyahama makaazi yao.

Msemaji wa ujumbe wa wafuasi wa Riek Machar, Yohannis Musa Pouk, amebaini kwamba wamefikia hatua muhimu, bila hata hivo kutoa maelezo yoyote.