AFRIKA KUSINI-Mgomo

Wachimba migodi Afrika Kusini wasusia kazi

Wafanyakazi wa machimbo ya madini ya Platinum nchini Afrika Kusini
Wafanyakazi wa machimbo ya madini ya Platinum nchini Afrika Kusini RFI

Mgomo mkubwa zaidi wa wafanyakazi wa machimbo ya madini ya Platinum nchini Afrika Kusini umepangwa kuanza hii leo siku ya Alhamisi Afrika Kusini, wakati awali Chama cha wafanyakazi wa ujenzi na migodini AMCU kilitoa wito kwa Wafanyakazi takribani elfu themanini Kususia kazi mwanzoni mwa Juma hili na kuelezea kuwa haimaanishi kuwa watasitisha mgomo wao mapema mno, kwa kuwa madai yao yanaendelea kupuuziliwa na serikali.

Matangazo ya kibiashara

Makampuni hayo yalipendekeza nyongeza ya asilimia 6.5 kiwango ambacho wafanyakazi hao wanadai hakitoshi na wanataka kifikie asilimia 10 ambayo ni sawa na asilimia 60 ya mshahara halisi.

Kizaazaa kimezuka sehemu mbalimbali Afrika Kusini, wafanyakazi wa migodini na viwandani wakisusia kazi mpaka hapo watakapoongezewa mishahara. Madereva wa magari makubwa nao wagoma hii leo.

Wimbi la mgomo wa wafanyakazi nchini Afrika Kusini linaendelea kuchukua sura mpya kila uchao ambapo sasa Kampuni ya Toyota mjini Durban imesitisha shughuli zake kwa siku ya nne leo. Pia, chama cha wafanyakazi wa usafirishaji nacho kinawachochea wanachama wake wa reli na bandari kujiunga na wimbi hilo.

Zaidi ya madereva 20,000 wa magari makubwa wanatarajiwa nao kuitikia wito huo ambao unalenga kuizorotesha kabisa sekta ya usafirishaji nchini Afrika Kusini.

Mgomo huo wa madereva ulioitishwa hii leo umeathiri sekta ya usambazaji wa mafuta na ugavi kwa kiasi kikubwa. Na kama mgomo huo utajumuisha pia wafanyakazi wa reli na bandari utaathiri vikubwa biashara ya kupeleka nje bidhaa kama vile makaa ya mawe, platinum na dhahabu.

Migomo hii yaathiri uzalishaji viwandani na hivyo kuzorotesha uchumi wa taifa.
Kampuni ya magari ya Toyota imesema imelazimika kufunga kiwanda chake cha magari cha nchini Afrika Kusini kwa siku nne kutokana na mgomo usio halali wa kudai nyongeza ya mshahara, wimbi lililoanzishwa na wafanyakazi wa migodini ambalo sasa linatapakaa nchi nzima.

Viongozi wa vyama vya wafanyakazi katika kiwanda hicho kikubwa mjini Durban wamesema wafanyakazi watarejea kazini Ijumaa ya leo baada ya kuongezewa mshahara kwa asilimia 5.4.