JAMUHURI YA AFRIKA YA KATI-Kiapo

Rais mpya wa mpito nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati aanza rasmi majukumu yake ya urais

Catherine Samba-Panza, rais mpya wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, akiwa pamoja na Laurent Fabius, waziri wa mashauri ya kigeni wa Ufaransa.
Catherine Samba-Panza, rais mpya wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, akiwa pamoja na Laurent Fabius, waziri wa mashauri ya kigeni wa Ufaransa. REUTERS/Siegfried Modola

Akikabiliwa na changamoto ya kuhakikisha usalama unarejea nchini mwake pamoja na kuleta umoja wa kitaifa, rais mteule wa mpito nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, Catherine Samba-Panza hapo jana ameapishwa rasmi kuanza kibarua cha kutumikia taifa hilo. Benki ya dunia tayari imeahidi kukusanya kiasi cha dola milioni 100 kusaidia kuinua uchumi wa taifa hilo ambao umeendelea kudorora kutokana na kushuhudiwa kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Matangazo ya kibiashara

Punde mara baada ya kuapishwa, rais Catherine Samba-Panza amesema huu ni muda wa kufanya kazi na kuagiza wananchi kurejea kwenye majukumu yao kuanzia jumatatu ya juma lijalo na kuagiza makundi ya watu wenye silaha kusalimisha silaha zao.
“Ili kuunga mkono jitihada za serikali itakayoundwa hivi karibuni baada ya mashauriano ya kina, naomba kwa msisitizo wapiganaji wa zamani wa seleka na anti-balaka kuonyesha uzalendo wao kwa kuweka mara moja chini silaha zao. hatutavumilia tena kuwepo kwa vurugu endelevu nchini”, amesema rais Samba-Panza.

Kwa upande wake nchi ya Ufaransa ambayo inawanajeshi zaidi ya elfu 1 na 500 nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, inasema inamatumaini makubwa ya kuona taifa hilo likirejea kwenye hali ya kawaida.
Francois Hollande ni rais wa Ufaransa.

“Leo ni tarehe 23 Januari na pia ni siku ambapo rais mpya wa jamhuri ya Afrika ya Kati anaapishwa. Hii ni ishara ya matumaini kuwa mchakato wa maridhiano utanza, hali ya usalama itarejea taratibu, na wananchi wataepushwa na majanga ya njaa, lakini mbaya zaidi na unyanyasaji”, amesema rais Hollande.

Awali Umoja wa mataifa UN ulitoa wito kwa viongozi wa mataifa ya Afrika Kuongeza wanajeshi zaidi wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya kati ili kulinda raia na kuzuia kile ambacho wataalamu walionya kuwa huenda taifa hilo likakumbwa na mauaji ya halaiki.
Ni wanajeshi elfu 4 pekee wa Umoja wa Afrika ambao wako nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kati ya wanajeshi elfu 6 ambao mataifa ya Afrika yaliahidi kupeleka wanajeshi wao huku nchi ya Ufaransa yenyewe ikiwa na wanajeshi elfu 1 na 500.
Waziri wa mawasiliano wa nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Adrien Pousson alisema juzi kuwa nchi yake itahudhuria mkutano ulioandaliwa na Jumuiya ya Kimataifa mjini Roma kwa lengo la kufikia maridhiano ya kitaifa.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanaona kuwa ni lazima rais mpya aweke mazingira mazuri ambayo yataondoa mgawanyiko wa kisiasa kwenye taifa hilo.

Machafuko yalilolikumba taifa hilo yamesababisha maefu ya raia kupoteza maisha na mamia kwa maelfu kuyahama makaazi yao.