SUDANI KUSINI-Mazungumzo

Serikali ya Sudan Kusini na waasi wakubaliana kusitisha mapigano

Wajumbe wa serikali ya Sudan Kusini na wale wa waasi wakiondoka ukumbini baada ya kusaini mkataba wa usitishwaji vita
Wajumbe wa serikali ya Sudan Kusini na wale wa waasi wakiondoka ukumbini baada ya kusaini mkataba wa usitishwaji vita RFI

Viongozi wa utawala wa Sudan Kusini na wale wa upande wa waasi, hatimaye wametiliana saini kusitisha mapigano ndani ya saa 24 na kumaliza wiki tano za mapigano yaliyoshuhudia maelfu ya raia wake wakiihama nchi yao. Ni uamuzi uliokuwa unasubiriwa kwa hamu na Jumuiya ya Kimataifa ambayo mara zote imekuwa ikizishinikiza pande hizo mbili kufikia makubaliano ya awali ambayo kwanza yalitaka kusitishwa kwa mapigano nchini humo ili kutoa nafasi ya mazungumzo zaidi ya amani kupata muafaka.

Matangazo ya kibiashara

Mkataba huu wa makubaliano ulitiwa saini na wawakilishi wa serikali ya rais Salva Kiir na wale wa upande wa waasi wanaomuunga mkono aliyekuwa makamu wa rais Riek Machar, makubaliano ambayo yalipokelewa kwa shangwe kwenye ukumbi uliotumika kufanyika shughuli hiyo.

Kwenye makubaliano haya, serikali ya rais Salva Kiir pia imekubali kuwaachia huru wafungwa 11 wa kisiasa walioko karibu na Riek Machar ambao walikamatwa punde baada ya kuzuka mapigano december 15 mwaka jana licha ya kuwa hakukuwa na muda maalumu wa makataa ya kuachiwa kwa wafungwa hao.

Ujumbe wa usuluhishi toka nchi wanachama za IGAD ambao walikuwa wanasimamia mazungumzo hayo wameeleza kuridhishwa na hatua hii muhimu iliyofikiwa na pande hizo mbili ambapo sasa kutasaidia kuwafikia maelfu ya raia kwenye miji iliyokuwa kwenye mapigano kutoa msaada wa kibinaadamu.

Nchi ya Marekani imekuwa taifa la mwanzo kupongeza uamuzi uliofikiwa mjini Addis Ababa Ethiopia na kutoa wito wa kufikia suluhu ya kudumu nchini humo ili kunusuru mauaji zaidi ya raia wasio na hatia.