UKRAINE

Rais wa Ukraine awapa wapinzani nafasi za uongozi serikalini ili kutuliza ghasia za waandamanaji

Reuters/David Mdzinarishvili

Wapinzani nchini Ukraine wameapa kuendelea na maandamano dhidi ya serikali ya Rais Viktor Yanukovych mpaka matakwa yao yatakapokamilika licha ya rais huyo kutoa nafasi za juu za uongozi kwa viongozi wa upinzani.

Matangazo ya kibiashara

Jana jumamosi, Rais Yanukovych alitangaza kutoa nafasi ya Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu viongozi wakuu wa upinzani Arseniy Yatsenyuk and Vitali Klitschko ili kujaribu kutafuta suluhu ya machafuko hayo yaliyodumu kwa takribani miezi miwili.

Wakizungumza na maelfu ya waandamanaji mjini Kiev, viongozi hao wa wapinzani wamesema lengo lao sio tu nafasi za uongozi serikalini bali ni kutaka Taifa hilo lijiunge na ushirikiano wa kiuchumi na Umoja wa Ulaya EU.

Bado haijafahamika kama viongozi hao watakubali kushika nyadhifa hizo ama watazikataa na kuendeleza harakati zao.

Umoja wa Ulaya umeomba zichukuliwe hatua madhubuti kusitisha ghasia hizo, ambazo kwa mujibu wa wanaharakati tayari zimesababisha vifo vya watu watano na huenda hali ikawa mbaya zaidi endapo Rais Viktor Yanukovych ataamua kutumia nguvu zaidi kukabiliana na makundi ya waandamanaji walioingia mitaani takribani miezi miwili sasa.

Polisi wameendelea kukabiliana na waandamanaji katika mji mkuu wa nchi hiyo Kiev wakitumia risasi za mipira na mabomu ya kutoa machozi hatua ambayo haijaonekana kufua dafu katika kutuliza ghasia.