JAMHURI YA AFRIKA YA KATI-Siasa

Jamhuri ya Afrika ya Kati imepata Serikali mpya

André Nzapayéké, waziri mkuu mpya wa Jamhuri ya Afrika ya Kati
André Nzapayéké, waziri mkuu mpya wa Jamhuri ya Afrika ya Kati RFI

Hatimae waziri mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya kati André NZAPAYEKE ameunda jana serikali yake mpya ya mpito inayojumuisha pande zote hususan waasi wa zamani wa Seleka na wanamgambo wa kikristo wa Anti-balaka. Serikali mpya hiyo ina mawaziri ishirini wakiwemo wanawake saba, kulingana na mwongozo wa rais Catherine Samba-Panza, sura ambayo inzungumziwa na waziri mkuu André NZAPAYEKE kuwa ya Kuridhisha

Matangazo ya kibiashara

Wakati huohuo, waasi wa zamani wa seleka wapatao mia sita wameondolewa jana kwenye kambi yao ya msingi na kuhamishwa, chini ya ulinzi wa askari wa Ufaransa wa Operesheni iliyobatizwa “Sangaris”, na kupelekwa nje kidogo ya mji mkuu Bangui kwa ajili ya usalama wa viongozi wapya.

Kanali Narkoyo mmoja wa waasi wa zamani wa Seleka, amesema kwamba wamwtii amri waliyopewa ya kukusanya wapiganaji wao, na kwa sasa wameondoka.

“Kama mnavyofahamu nchi hii inaongozwa na mamlaka ya aina tofauti, tumeamriwa na vikosi vya MISCA na Operesheni sangaris kuwakusanya askari wetu, tumefanya hivyo na kuwahamishia kwenye kambi ya RDT”, amesema kanali Narkoyo.

Wachambuzi wa masuala ya Kisiasa wanazungumzia hatua hiyo kuwa njia ya kuruhusu viongozi wapya na vikosi vya kimataifa kutekeleza majukumu yao bila ya vizuwizi vyovyote.

wakati hayo yakijiri, hali ya usalama katika Jamhuri ya Afrika ya Kati inaendelea kuwa mbaya licha ya kuwepo kwa rais mpya Bi Catherine Samba-Panza.
Mkuu wa shirika la Haki za binadamu katika umoja wa Mataifa Navi Pillay amesema kuwa Jumuiya ya Kimataufa inastahili kutuma wanajeshi zaidi nchini humo ili kulinda amani.