MAREKANI-SYRIA

Rais wa Syria, Bashar al-Assad aonywa kuhusu makubaliano ya uteketezaji wa silaha za kemikali

REUTERS

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amemuonya Rais wa Syria Bashar al-Assad kuwa atakabiliwa na matokeo mabaya kutokana na kushindwa kutekeleza makubaliano ya kuondoa silaha za kemikali kama ilivyokubaliwa hapo awali.

Matangazo ya kibiashara

Kerry ametoa kauli hiyo mjini Berlini Ujerumani baada ya kumaliza mazungumzo yake na Kansela Angela Merkel ambapo amesema wanajua kuwa utawala wa Assad unaondoa silaha hizo kwa mwendo wa kinyonga tofauti na makubaliano yanavyosema.

Shirika linalodhibiti kemikali la Umoja wa Mataifa juma hili lilisema serikali ya Damascus imewasilisha chini ya silimia 5 ya silaha zake za maangamizi kwa ajili ya kuteketezwa.

Takribani tani 700 za silaha za kemikali zilitakiwa kuondolewa nchini Syria kabla ya tarehe 31 mwezi Desemba mwaka jana lakini jitihada hizo bado hazijakamilika.

Waziri Kerry pia amekutana na Waziri wa mambo ye nje wa Urusi Sergei Lavrov pambezoni mwa mkutano wa usalama mjini Munich ambapo viongozi hao wamejadili awamu ijayo ya mazungumzo ya amani kuhusu Syria yaliyopangwa kufanyika tena tarehe 10 mwezi huu.

Awamu ya kwanza ya mazungumzo hayo ilitamatika jana ijumaa mjini Geneva Uswisi ambapo mpatanishi mkuu wa mgogoro huo, Lakhdar Brahimi alikiri kuwa mazungumzo hayo yamekuwa magumu licha ya pande zote mbili kuonesha nia ya kutaka kufikia suluhu ya machafuko.