Jeshi la kulinda amani Jamuhuri ya Afrika ya Kati lafanikiwa kurejesha udhibiti wa mji wa Sibut uliotekwa na waasi
Imechapishwa:
Jeshi la kulinda amani huko jamuhuri ya Afrika ya kati limefanikiwa kuurejesha mikononi mwao mji wa Sibut uliokuwa ukidhibitiwa na wapiganaji waasi wakati huu mpango wa kuongeza nguvu katika jeshi hilo ukifanikiwa kukusanya dola za Marekani milioni 132 kutoka mataifa ya Afrika.
Kamanda wa jeshi la Umoja wa Afrika Tumenta Chomud aliimbia radio ya taifa hilo kuwa jeshi lake limedhibiti mji uliokuwa chini ya wapiganaji waasi wa kiislamu seleka waliopindua serikali mnamo mwezi machi 2013 na kulitumbukiza taifa hilo katika mzozo.
Hayo yanajiri wakati hapo jana jumamosi viongozi wa bara la Afrika na wanadiplomasia wa kimataifa wamefanikisha zoezi la kuchangia pesa jeshi la umoja wa Afrika chini ya operesheni yake MISCA ambayo inatarajiwa kuongeza wanajeshi takribani elfu sita kufikia mwezi machi mwaka huu.
Aidha Viongozi wa nchi za Afrika walikubaliana kuendelea kuchukua hatua zaidi kudhibiti machafuko yanayozikumba nchi wanachama sambamba na kuunda kikosi cha dharura kitakachoshughulikia migogoro inayolikumba bara hilo, azimio hilo limefikiwa jana katika siku ya mwisho ya mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika AU mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Viongozi walioshiriki mkutano huo wa siku mbili wametaka kuchukuliwa kwa hatua za haraka ili kuikoa nchi ya Sudani Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati ambazo zinakumbwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti mpya wa AU ambaye ni Rais wa Mauritania, Mohamed Ould Abdel Aziz amesema nchi wanachama zitatoa wanajeshi watakaounda kikosi hicho.