SUDANI KUSINI-Usalama

Wanajeshi wa Sudan Kusini watuhumiwa kupora vifaa vya shule

Wanajeshi wa Sudan Kusini, mjini Juba
Wanajeshi wa Sudan Kusini, mjini Juba RFI

Shirika la Umoja wa Mataifa linalo hudumia watoto duniani, UNICEF, limevituhumu vikosi vya serikali ya Juba kwa kuendesha uporaji wa vifaa vya shule vya watoto katika ofisi zake. Si kwa mara ya kwanza wanajeshi wa serikali ya Juba wanatuhumiwa kutekeleza baadhi ya vitendo viovu.

Matangazo ya kibiashara

Tuhuma hizo zinakuja baada ya picha za wanajeshi wa Sudani Kusini kuzagaa katika mitandao wakionekana wamebeba vifaa vya watoto vya shule vinavyotolewa na shirika hilo la UNICEF na ambavyo vimeandikwa Rejea Shuleni.

Kwa mujibu wa msemaji wa shirika la UNICEF, Sarah Crowe amesema vifaa vingi vya watoto vimeporwa katika maeneo mengi nchini Sudani Kusini wakati wa vita na kuongeza kwamba hii inamaanisha kwamba hata serikali ya Juba haiheshimu kanuni na taratibu za Umoja wa Mataifa juu ya misaada ya kibinadamu.

Wanajeshi wa rais Salva Kiir na waasi wanaomtii makamu wa rais wa zamani Riek Mashar wanatuhumiwa kuendesha uporaji wa vifaa mbalimbali vya mashirika ya misaada hususan magari, chakula na madawa.

Mapigano kati ya jeshi la Sudan Kusini na waasi wanaomuunga mkono Riek Machar yamesababisha maelfu ya raia kupoteza maisha na mamia kwa maefu kulazimika kuyahama makaazi yao.