Burundi - Siasa

Hali ya kisiasa nchini Burundi yaendelea kuchacha wakati huu mawaziri kutoka chama Uprona wakijiuzulu

Jean Claude Ndihokubwayo waziri wa maendeleo ya wilaya aliye jiuzulu nchini Burundi
Jean Claude Ndihokubwayo waziri wa maendeleo ya wilaya aliye jiuzulu nchini Burundi IWACU

Hali ya kisiasa nchini Burundi imeendelea kuwa tete, kufuatia taarifa za kujiuzulu kwa waziri mwingine wa serikali toka chama kikuu cha upinzani, UPRONA hali inayoendelea kuleta sintofahamu kati yake na chama tawala cha CNDD-FDD.Taarifa za hivi karibuni zinasema kuwa waziri wa maendeleo ya wilaya, Jean Claude Ndihokubwayo ametangaza kujiuzulu kwa kile kinachodaiwa kuwa ni hatua ya rais kutangaza kumfuta kazi aliyekuwa makamu wake wa kwanza wa rais Bernard Busokoza mwishoni mwa juma lililopita.

Matangazo ya kibiashara

Mbali na kutangaza kujiuzulu kwa waziri huyo, ameweka wazi kwamba hatokubali pendekezo la kumteuwa kuwa makamu wa rais wa nchi hiyo.

Wakati huo huo waziri wa habari Concilie Nibigira amejiuzulu pia kufuatia tuhuma za chama tawala kushindwa kushirikiana vilivyo na cha UPRONA.

Kufutwa kazi kwa makamu wa kwanza wa rais nchini Burundi kumezua mjadala mkubwa nchini humo, hatuwa ambayo imekuja miezi michache kabla ya kufutwa kazi kwa aliyekuwa mtangulizi wake Bernard Busokoza.

Mwishoni mwa juma lililopita waziri wa mambo ya ndani nchini humo Edouard Nduwimana alibadilisha maamuzi katika chama cha UPRONA na kutangaza kutoutambuwa uongozi wa sasa wa chama hicho, wa Charles Ntitije, na kuweka wazi kwamba serikali inautambuwa utawala wa Niyoyankana.

Hatuwa iliopelekea makam wa rais Bernard Busokoza kutoka chama hicho kuingilia kati na kubadilisha uamuzi huo wa waziri wa mambo ya ndani na kumtuhumu kuingilia ndani mzozo wa chama chake bila hata hivyo kujadiliana naye.

Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa kuna hatari ya kutokea mzozo kwenye Serikali ya Chama tawala kufuatia kuendelea kujiuzulu kwa mawaziri zaidi toka chama cha UPRONA ambacho kinaunda serikali na chama tawala cha CNDD-FDD.

UPRONA na FRODEBU-NYAKURI ni vyama viwili pekee kati ya vyama 10 vikuu vya upizani ambavyo havikususia uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ulioshuhudia kusalia madarakani kwa rais Nkurunzinza ambapo vyama vingine vyote vilisusia uchaguzi huo.