Burundi - Siasa

Mchakato wa kumtafuta makamo mpya wa kwanza wa rais unaendelea nchini Burundi

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza
Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza RFI

Nchi ya Burundi imeendelea kutumbukia kwenye mzozo zaidi wa kisiasa kufuatia kuendelea kujiuzulu kwa mawaziri na viongozi mbalimbali toka chama kikuu cha upinzani cha Uprona chenye asili ya jamii ya Kitutsi kilichokua kikishirikiana serikalini na chama tawala cha CNDD-FDD chenye asili ya jamii ya wahutu. 

Matangazo ya kibiashara

Mawaziri watatu kutoka chama cha UPRONA mwamejiuzulu baada ya chama wanakotoka kuwataka wafanye hivo, baada ya rais wa Burundi kuchukua hatua mwishoni mwa juma liliyopita ya kumfuta kazi makamu wake wa kwanza Bernard Busokoza. Bernard Busokoza alifutwa kazi, baada ya kuchukua hatua ya kufuta hatua ya waziri wa mambo ya ndani Edouard Nduwimana ya kutomtambua Charles Nditije kama kiongozi wa chama cha UPRONA na badala yake kumtambua Bonaventure Niyoyankana kama kiongozi halali wa chama hicho.

Bernard Busokoza alimlaumu waziri wa mambo ya ndani kwamba alichukua hatua bila kumfahamisha wakati wizara hio iko chini ya mamlaka yake. Bernard Busokoza alibaini kwamba hatua hio ya waziri wa mambo ya ndani ilikua na lengo la kuchochea uhasama na vurugu katika chama UPRONA.

Kamati kuu ya chama cha UPRONA pamoja na wabunge kutoka chama hicho wanabaini kwamba utawala wa CNDD-FDD una lengo la vunja chama cha UPRONA. Mawaziri hao waliyojiuzulu ni pamoja na waziri wa maendeleo ya wilaya Jean-Claude Ndihokubwayo, waziri wa habari Leocadie Nihaza na waziri wa biashara na utalii Victoire Ndikumana ambae alipata tuzo tatu kutokana na juhudi zake katika masuala ya utalii.,

Hata hivyo rais wa Burundi kupitia naibu msemaji wake Willy Nyamitwe, amesema mchakato wa kumtafuta makamu wa kwanza mpya wa rais kutoka chama cha UPRONA unaendelea.

“Kinachohitajika kwa sasa ni kuharakia kumtafuta makamu wa kwanza wa rais, kwani wadhifa huo ni moja kati ya nguzo muhimu za serikali, kwa hio rais ana muda wa siku thelathini ili awe ameshamteua mtu kwenye nafasi hio”, amesema Willy Nyamitwe.

Hayo yanajiri wakati, ambapo nchi hiyo ikijiandaa na uchaguzi mkuu mwaka 2015.

Wachambizi wa mambo wameonya kuhusu kuendelea kushuhudiwa kwa mvutano huu wa kisiasa ambao huenda ukasababisha vurugu za kisiasa nchini humo.