Umoja wa Mataifa umewataka waasi wa FDLR kujisalimisha na Kurejesha silaha.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Hatimaye Umoja wa Mataifa umevunja ukimya wake na kujibu pendekezo la waasi wa Rwanda wa FDLR kufwatia nia yao ya kuweka silaha chini na kujisalimisha kwa ajili ya mazungumzo na serikali ya Kigali. Mbali na kauli zilizotolewa na waasi hao na kusikika kwenye vyomba mabimbali vya habari, vikosi vya kimataifa vya kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vinakitaka kikundi cha waasi cha FDLR kutekeleza kwa vitendo na ushahidi wa dhati nia waliyoionyesha hivi karibuni.
Mwakilishi maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Martin Kobler , akiwa pia mkuu wa vikosi vya MONUSCO, amesema, wapiganaji wa FDLR wanatakiwa tu kujisalimisha.
“Tunayo fursa moja tu. Ni fursa ya kujisalimisha. Pia ni wajibu wao wenyewe kuwasilisha silaha zao kwenye makambi yetu. Hii ndio sera yetu, hatutaruhusu hali yoyote ya kutowajibika na hatuna chochote cha kujadili”, amesema Kobler.
Wakati hayo yakijiri, zaidi ya familia elfu moja wamekimbia makazi yao siku za hivi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo maeneo ya Walikale na Lubero kufwatia machafuko yanayoendeshwa na waasi hao wilayani Lubero, jambo ambalo linalalamikiwa na mashirika ya kiraia wilayani humo.
Hata hivyo, waasi wa FDLR wanakanusha kuhusika na mashambulio ya hivi karibuni na kutuhumu serikali ya Rwanda kupanga vikundi vingine ili kukichafua kundi la waasi hao.
“Sio kweli kwamba ni wa FDLR, wako watu wengi ambao tayari wamenunuliwa na serikali ya Kigali kuvuruga amani ya raia na baadaye kunyooshea kidole kundi la FDLR”, amesema Kanali Wilson Nyirategeka, ambae ni Katibu Mtendaji wa waasi wa FDLR.
Hivi karibuni waziri mkuu wa zamani wa Rwanda Faustin Twagiramungu, alitangaza kwamba chama chake kimejiunga na kundi la waasi la wa kihutu wa Rwanda la FDLR. Lakini serikali ya Kigali inalituhumu kundi hilo kwamba lilihusika katika mauwaji ya kimbari yaliyotekea nchini Rwanda mwaka 1994, ambapo inasadikiwa kua watu 800,000 kutoka jamii ya watutsi na wahutu waliyokua wakipinga sera za utawala wa rais Juvenal Habyarimana waliuawa.