KENYA-ICC

Ushahidi waendelea kukosekana katika kesi inayomkabili rais wa Kenya

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta RFI

Wakili wa rais wa Kenya katika kesi inayo mkabili katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC Steven Kay amewambia majaji wa mahakama hiyo kwamba kesi hiyo haina mshiko tena. Muendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo bi Fatou Bensouda ameendelea kuituhumu serikali ya Kenya kwa kutoshirikiana kikamilifu na makahama hiyo hasa kwamba kwa sasa hakuna mashahidi wanaomtuhumu rais Kenyatta. Hali ambayo inayopelekea rais Kenyatta kuonekena kutokuwa na kesi.

Matangazo ya kibiashara

Kesi hiyo ya rais Kenyatta imeahirishwa mara kadhaa na ambapo ilikuwa isikilizwe mwishoni mwa mwezi uliopita wa Januari, lakini muendesha mashataka aliomba kuahirishwa na kiuomba muda wa miezi mitatu zaidi na kuthibitisha kuwa hana tena ushahidi baada ya kujiondowa kwa mashahidi wawili muhimu.

Kikao cha jana kati ya upande wa mashtaka na upande wa utetezi, kimefanyika kufuatia tarehe 23 ya mwezi january mwaka huu, ofisi ya mwendesha mashtaka kuwasilisha ombi kwenye mahakama hiyo kutaka kesi dhidi ya rais Kenyaata iliyokuwa imepangwa kuanza jana kusogezwa mbele kwa miezi mitatu zaidi.

Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo, Fatou Bensouda alisema lengo la kutaka kuahirishwa kwa kesi hiyo ni kutokana na kuondolewa na kujiondoa kwa mashahidi muhimu kwenye kesi hiyo pamoja na kukosa ushirikiano toka serikali ya Kenya na hivyo kutaka muda zaidi wa kukusanya ushahidi.

Upande wa utetezi umekua ukiwataka majaji wa mahakama hiyo, kutupilia mbali kesi dhidi ya mteja wao kwa madai kuwa ofisi ya mwendesha mashtaka haina ushahidi wa kutosha kuendelea na kesi dhidi ya rais Uhuru Kenyatta.

Rais Kenyatta anashtakiwa na mahakama ya ICC kwa kuhusika kufadhili kuchochea na kupanga machafuko ya baada ya uchaguzi nchini Kenya mwaka 2007 na kusababisha zaidi ya watu elfu moja kupoteza maisha na maelfu kukimbia makwao.

Kesi ya naibu wake William Ruto na mwanahabari Joshua Arap Sang inaendelea kusikilizwa katika mahakama hiyo.