AFRIKA KUSINI-Mgomo

Mkutano wa kujaribu kumaliza mgomo wa wafanyakazi kwenye migodi unafanyika kesho Afrika Kusini

Wafanyakazi wa machimbo ya madini ya Platinum nchini Afrika Kusini wakianadamana
Wafanyakazi wa machimbo ya madini ya Platinum nchini Afrika Kusini wakianadamana RFI

Wafanyakazi kwenye migodi nchini Afrika Kusini wanataraji kukutana kesho Jumanne na upande wa upatanishi ili kujaribu kumaliza mgomo huo ambao umedumu kwa majuma mawili sasa. Mazungumzo hayo yalisitishwa ghafla Jumatano iliopita baada ya kukosekana muafaka baina ya waajiri na wafanyakazi.

Matangazo ya kibiashara

Kamati ya maridhiano inayoendesha mazungumzo hayo itakutana falagha na Kamati ya wafanyakazi wa migodini.

Takriban wafanyakazi elfu thamanini wa shirika la wafanyakazi wa migodini walianza mgomo tangu Januari 23 wakiomba nyongeza ya mshahara wa randi 12,500 sawa na Euro 830, ikiwa ni mara mbili ya mshahara wanaoupata kwa sasa. Kampuni za uchimbaji migodi zilitowa asilimia 7 ya nyongeza ya mshahara, Jambo ambalo lilitupiliwa mbali na wafanyakazi hao.

Awali Chama cha wafanyakazi wa sekta ya madini nchini Afrika Kusini AMCU kilisema kuwa zaidi ya wafanyakazi elfu sabini wataendelea na mgomo hadi matakwa yao yatakapotimizwa.

Afrika Kusini inakabiliwa mara kwa mara na migomo ya Wafanyakazi wa machimbo ya madini. Kwa sasa sekta ya uchimbaji wa madini ya Platinum inakumbwa na kizaaza tangu mkasa wa mwaka juzi wa Marikana ambapo wachimba migodi wapatao 34 walipigwa risasi na polisi walipokuwa wakiandamana kuendeleza mgomo wao, uliotajwa na serikali kuwa haramu.

Safari hii mgomo huu wa kudai nyongeza ya mishahara unaongozwa na AMCU chama chenye msimamo mkali cha kutetea haki ya wafanyaki wa migodini na mafundi katika sekta ya ujenzi.

Wachimba migodi hao ambao hufanya kazi kwenye machimbo ya kina kirefu sana, wanadai mishahara ya takriban randi 12,500 kwa mwezi sawa na Euro 830 , ikiwa ni maradufu ya mishahara wanayopokea sasa.

Tofauti na mgomo wa Marikana, mgomo huu ulyokua ukiendelea ni halali kisheria.
Awali kampuni zote tatu za Anglo American, Impala na Lonmin Platinum zinazomiliki wafanyakazi hao zilidai kwamba haziwezi kumudu kulipa nyongeza hiyo inayodaiwa kwa sababu ya gharama za uzalishaji ni kubwa na mauzo ni haba.

Afrika Kusini ndio nchi inayozalisha madini ya Platinum kwa wingi zaidi huku asilimia 80% ya madini hayo yakiwa bado hayajachimbwa.