MAREKANI-SYRIA-URUSI

Marekani yaitaka Urusi kuishawishi serikali ya Damascus kushiriki kikamilifu mazungumzo ya amani kuhusu Syria

REUTERS/Denis Balibouse

Marekani imeitaka serikali ya Urusi kushinikiza upande wa serikali ya Syria kushiriki kikamilifu mchakato wa upatikanaji wa amani baina yao na waasi, kauli ambayo inakuja baada ya kutamatika kwa mazungumzo ya amani mjini Geneva Uswisi bila matumaini yoyote ya pande hizo kufikia suluhu.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Washington Marie Harf amesema utawala wa Moscow unatakiwa kuishinikiza zaidi Damascus baada ya wajumbe wake katika mazungumzo hayo kukataa kujadili maswala yoyote nje ya ugaidi huku wakiwalaumu wapinzani wao na mataifa yanayowaunga mkono kuwa chanzo uvunjifu wa amani.

Mazungumzo ya Geneva II kuhusu amani ya Syria yalianzishwa kwa ushirikiano wa Marekani inayounga mkono Muungano wa upinzani pamoja na Urusi wanaoiunga mkono serikali ya Rais Bashar al-Assad, lakini jitihada hizo hazijafanikiwa kuzishawishi pande kinzani kufikia suluhu.

Mpatanishi wa mgogoro huo Lakhdar Brahimi amewaalika wawakilishi wa pande zote katika mkutano wa mwisho leo jumamosi asubuhi.

Bado haijafahamika wajumbe hao watakubali kurejea tena mjini Ganeva katika awamu ya tatu ya mazungumzo hayo.

Wakati huo huo mapigano yamekuwa yakiendelea nchini Syria katika majuma ya hivi karibuni, wakati Mkuu wa maswala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Valerie Amos akitoa wito kwa baraza la usalama la umoja huo kuhakikisha misaada zaidi inafikishwa nchini Syria.